Williams ajifunga kitanzi Bilbao

BILBAO, Winga wa Athletic Bilbao Nico Williams amesaini mkataba mpya wa miaka nane kuendelea kusalia klabuni hapo hadi mwaka 2035 akisititisha tetesi za muda mrefu zilizomhusisha winga huyo na Mabingwa wa Laliga FC Barcelona.
Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Athletic Bilbao zinaeleza kuwa klabu pia imeongeza kiwango cha pesa kwenye kipengele chake cha kumuachilia kwa 50% huku kukiwa na ripoti kuwa kipengele cha awali kilikuwa na thamani ya karibu Euro milioni 62.
“Linapokuja suala la kufanya maamuzi kwangu jambo la muhimu ni kuusikiliza moyo. Nipo ninapotaka kuwa, na watu wangu kwa sababu hapa ni nyumbani” – amesema Williams katika taarifa ya klabu hiyo
Mhispania huyo mwenye miaka 22 ambaye mkataba wake wa awali ulikuwa ukitamatika mwaka 2027 ni moja ya nyota wanaohusudiwa sana katika klabu hiyo akiwa amecheza michezo 167 kwenye mashindano yote.
Mwezi uliopita Athletic iliwakemea vikali mashabiki waliofuta picha za kuchora za Nico na kaka yake Inaki ambaye pia anacheza klabuni hapo baada ya mashabiki hao kukasirika kufuatia tetesi za nyota huyo kuondoka zilizokolezwa moto na maneno ya mkurugenzi wa michezo wa Barcelona Deco aliyesema wanalenga saini ya winga huyo.