Muziki

Diamond, Zuchu, Abby Chams Wang’ara Tuzo za AFRIMMA 2026

DAR ES SALAAM: WASANII wa muziki kutoka Tanzania wameendelea kuonesha ushindani katika jukwaa la kimataifa baada ya jumla ya wasanii 11 kutajwa kuwania tuzo za African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2026, zitakazofanyika Septemba 12, 2026, jijini Dallas, Texas, Marekani.

Kwa mujibu wa waandaaji wa tuzo hizo, Tanzania imepata uwakilishi mkubwa katika vipengele mbalimbali, ikiwemo vya muziki wa Bongo Fleva, Injili, uongozaji wa video na uchezaji.

Katika kipengele cha Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki, wanaowania tuzo kutoka Tanzania ni Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, Juma Jux, Barnaba Classic, Mbosso Khan na Marioo.

Kwa upande wa Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki, Tanzania inawakilishwa na Zuchu pamoja na Abigail Chams (Abby Chams), ambao watachuana na wasanii wengine kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika kipengele cha Mwongozaji Bora wa Video (Best Video Director), Hanscana amepewa nafasi ya kuwania tuzo hiyo kutokana na mchango wake katika tasnia ya video za muziki.

Kwa upande wa muziki wa Injili, Christina Shusho na Joel Lwaga wameingia katika orodha ya wanaowania tuzo, wakiiwakilisha Tanzania katika kipengele hicho.

Aidha, mwanadansi Angel Nyigu ndiye Mtanzania pekee aliyefanikiwa kutinga katika kipengele cha Mnenguaji Bora (Best Dancer), ambapo atachuana na wanadansi kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika, akiwemo kundi la Ghetto Kids kutoka Uganda na Hope Ramafalo.

Washindi wa tuzo za AFRIMMA 2026 wanatarajiwa kutangazwa katika hafla itakayofanyika Septemba 12, 2026, jijini Dallas, Marekani, huku Tanzania ikitarajia kufanya vyema kupitia wasanii wake wanaowania tuzo hizo.

Related Articles

Back to top button