Filamu

Watengeneza filamu Nigeria wakimbilia YouTube

LAGOS: SEKTA ya filamu nchini Nigeria (Nollywood) inaendelea kushuhudia mabadiliko makubwa huku watengenezaji wengi wa filamu wakichagua kuachana na sinema na majukwaa ya kulipia kama Netflix na Amazon Prime, na kuelekeza kazi zao moja kwa moja kwenye YouTube.

Hatua hiyo imefungua fursa mpya kwa kizazi kipya cha watayarishaji wa filamu wanaotafuta uhuru wa ubunifu na njia mbadala za kupata mapato.

Miongoni mwao ni mkurugenzi David Akwayo mwenye umri wa miaka 28 ambaye anajiandaa kuzindua filamu yake mpya ya ‘Diary of a Lagos Girl’ kupitia YouTube baada ya miaka kadhaa ya kufanya kazi za malipo madogo katika tasnia hiyo Nollywood.

Akwayo amesema YouTube imempa nafasi ya kufikia watazamaji moja kwa moja bila kutegemea wadau wachache waliokuwa wakidhibiti sekta hiyo.

Kwa mujibu wa wadau wa tasnia hiyo, filamu zinazowekwa YouTube zinaendelea kuvutia watazamaji wa mamilioni, huku mapato yakitokana na matangazo yanayoonyeshwa kabla na wakati wa video.

Hata hivyo, baadhi ya wakongwe wa tasnia hiyo wameonya kuwa kukimbilia mapato ya haraka kunaweza kushusha ubora wa kazi zinazozalishwa.

Licha ya changamoto hizo, wachambuzi wanaamini kuwa ukuaji wa matumizi ya intaneti pamoja na watazamaji kutoka diaspora unaifanya YouTube kuwa moja ya majukwaa yenye ushawishi mkubwa katika mustakabali wa filamu duniani.

Related Articles

Back to top button