Kenya yatwaa tuzo ya kwanza ya dhahabu Jumuiya ya Madola

SCOTLAND: Kenya imeandika historia kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola 2026 (Commonwealth Games) inayoendelea jijini Glasgow, Scotland, baada ya Edmund Serem kuipa nchi hiyo medali yake ya kwanza ya dhahabu kwa kuongoza ushindi wa kihistoria wa Wakenya wote watatu katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji (Steeplechase).
Serem, ambaye ni bingwa wa dunia kwa vijana chini ya miaka 20, alitumia dakika 8:18.23 kutwaa medali ya dhahabu. Mwenzake Simon Koech alimaliza wa pili kwa muda wa 8:18.59 na kujinyakulia fedha, huku Leonard Bett akichukua shaba kwa muda wa 8:21.63, na kuifanya Kenya kutawala washindi.
Ushindi huo umeongeza idadi ya medali za Kenya kufikia tano, zikiwemo dhahabu moja, fedha mbili na shaba mbili, baada ya Diana Wanza kutwaa fedha katika mbio za wanawake za mita 10,000 mapema siku jana.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Serem alisema ametimiza ndoto yake kwa kutwaa ubingwa katika ushiriki wake wa kwanza mashindano ya Jumuiya ya Madola.
“Nimetwaa taji langu la kwanza kwenye Commonwealth Games zangu za kwanza na nina furaha kubwa. Najua familia yangu nyumbani ina furaha, pamoja na Wakenya wote. Zaidi ya yote tumefanikisha ushindi wa nafasi tatu za juu kwa Kenya,” alisema Serem.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 20 alikiri kuwa hakutarajia kushinda kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo, akiwemo bingwa wa dunia wa New Zealand Geordie Beamish pamoja na Simon Koech ambaye hivi karibuni alikimbia chini ya dakika nane.
“Nilikuwa na matumaini ya kupanda jukwaani lakini sikuwa na uhakika wa kushinda. Nilipoingia mzunguko wa mwisho nilihisi bado nina nguvu, ndipo nikaamua kuongeza kasi hadi nikafanikiwa kushinda,” aliongeza.
Kwa miaka mingi Kenya imeendelea kutawala mbio za steeplechase duniani kupitia mabingwa kama Ezekiel Kemboi, Conseslus Kipruto, Brimin Kipruto na Saif Saaeed Shaheen, huku ushindi wa Glasgow ukithibitisha tena ubabe wa taifa hilo katika mbio hizo.



