Filamu

Funke avunja rekodi Nollywood Box Office

LAGOS: Muigizaji na mtayarishaji wa filamu wa Nigeria, Funke Akindele, ameendelea kuthibitisha nafasi yake kama mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika tasnia ya Nollywood baada ya filamu yake ‘Everybody Loves Jenifa’ kuvunja rekodi za mapato katika kumbi za sinema nchini Nigeria.

Filamu hiyo iliyotolewa rasmi Desemba 13, 2024, imekuwa moja ya mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Nollywood, baada ya kufikisha zaidi ya naira bilioni 1 (₦1bn) ndani ya siku 19 pekee tangu kuanza kuonyeshwa kwenye sinema. Mafanikio hayo yaliifanya kuwa filamu ya Nollywood iliyofikisha kiwango hicho kwa kasi zaidi wakati huo.

“Everybody Loves Jenifa” ni sehemu ya mfululizo wa filamu maarufu za Jenifa ambao ulianza mwaka 2008 na kumjengea Funke Akindele umaarufu mkubwa kupitia mhusika wa Jenifa, mwanamke mwenye ndoto kubwa anayekabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.

Katika filamu hiyo, Funke Akindele siyo tu mwigizaji mkuu bali pia alihusika katika utayarishaji, jambo linaloonyesha uwezo wake wa kuendesha miradi mikubwa ya filamu kuanzia wazo hadi kufikisha kazi kwa watazamaji.

Mafanikio ya filamu hiyo yaliendelea kukua na baadaye kufikisha zaidi ya ₦1.8 bilioni kwenye mapato ya box office ya Nigeria, hatua iliyomfanya Funke kutajwa kama mmoja wa watayarishaji wenye mafanikio makubwa zaidi Afrika Magharibi.

Funke Akindele sasa anaingia kwenye orodha ya watengenezaji wachache wa Nollywood walioweza kuvuka mipaka ya Afrika na kuonyesha kuwa filamu za Nigeria zina uwezo wa kushindana katika soko la kimataifa.

Mafanikio yake yameongeza ushindani ndani ya Nollywood, huku watayarishaji wengine wakijaribu kufikia kiwango cha ubora na mapato alichoweka kupitia miradi yake mikubwa.

Related Articles

Back to top button