Burudani

TAVIC yapata leseni ya kwanza kusimamia mirabaha ya filamu Tanzania

DAR ES SALAAM: Kampuni ya Tanzania Audiovisual Collection Ltd (TAVIC) imekabidhiwa rasmi leseni ya kuwa Collective Management Organisation (CMO) ya kwanza kwa sekta ya kazi za sauti na picha (audiovisual) nchini.

Leseni hiyo inairuhusu TAVIC kukusanya na kusambaza mirabaha kwa wenye haki za kazi za filamu na maudhui mengine ya audiovisual, hatua inayotarajiwa kuimarisha usimamizi wa hakimiliki na kuhakikisha wabunifu wananufaika zaidi na kazi zao.

Kupatikana kwa leseni hiyo kunafuatia mchakato wa takribani miezi minne uliokuwa ukisimamiwa na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA).

Katika kipindi hicho, TAVIC ilitakiwa kutimiza masharti mbalimbali yaliyowekwa na mamlaka hiyo, ikiwemo kuweka dhamana ya Sh milioni 250 kabla ya kuidhinishwa kuanza shughuli zake rasmi.

Kwa leseni hiyo, TAVIC sasa ndiyo taasisi ya kwanza nchini yenye jukumu maalumu la kusimamia ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha kwa watayarishaji wa filamu, waongozaji, waigizaji na wadau wengine wa kazi za audiovisual.

Mfumo huo unatarajiwa kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na matumizi ya kazi za filamu kupitia vituo vya televisheni, majukwaa ya kidijitali, sehemu za burudani na watumiaji wengine wa maudhui hayo.

Kwa miaka mingi, jukumu la ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha lilikuwa likitekelezwa na COSOTA. Hata hivyo, marekebisho ya mfumo wa usimamizi wa hakimiliki nchini yamefungua fursa kwa kampuni binafsi zilizopewa leseni kufanya kazi hiyo kama Collective Management Organisations (CMOs), huku COSOTA ikiendelea kuwa msimamizi wa utoaji wa leseni na ufuatiliaji wa shughuli zao.

Wadau wa tasnia ya filamu wanaamini kuanza kwa shughuli za TAVIC kutasaidia wabunifu kupata stahiki zao kwa ufanisi zaidi, kuongeza thamani ya kazi za ubunifu na kuimarisha ulinzi wa hakimiliki nchini. Aidha, hatua hiyo inatarajiwa kutoa motisha kwa watayarishaji kuendelea kuwekeza katika utengenezaji wa filamu zenye ubora na ushindani mkubwa.

Kukabidhiwa kwa leseni hiyo ni sehemu ya mageuzi yanayoendelea katika sekta ya hakimiliki Tanzania, yenye lengo la kuhakikisha wasanii na wabunifu wananufaika ipasavyo na matumizi ya kazi zao kupitia mfumo wa kisasa, wenye uwazi na ufanisi katika ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha.

Related Articles

Back to top button