Riadha

Mwanariadha mwenye mguu bandia kuandika historia Marekani

LOS ANGELES: Mshindi wa medali tatu za Michezo ya Walemavu Duniani (Paralympic), Mohamed Lahna, yuko hatua za mwisho za kuandika historia baada ya kukaribia kukamilisha safari ya kipekee ya Triathlon Across America, akiwa mwanariadha wa kwanza mwenye mguu bandia kufanya triathlon ya kuvuka Marekani kwa umbali wa zaidi ya maili 3,300.

Lahna alianza safari hiyo Juni 13, 2026, akiwa na lengo la kuonyesha kuwa ulemavu si kikwazo cha kufikia mafanikio makubwa katika michezo ya uvumilivu.

Safari hiyo imehusisha hatua tatu za triathlon. Mwanzo alikamilisha kuogelea umbali wa maili 28.5 kuzunguka Kisiwa cha Manhattan jijini New York, kabla ya kuendesha baiskeli kwa zaidi ya maili 3,000 akipitia majimbo 16 ya Marekani.

Kwa sasa, mwanariadha huyo yuko kwenye hatua ya mwisho ya safari hiyo, akikimbia maili 350 kutoka Las Vegas, Nevada kuelekea Venice Beach, Los Angeles, ambapo anatarajiwa kumaliza safari yake Julai 29, 2026.

Licha ya kukabiliwa na joto kali la jangwani, uchovu wa safari ndefu na changamoto za kutumia mguu bandia wakati wa mbio, Lahna ameendelea kusonga mbele hatua kwa hatua, akionyesha mfano wa uthabiti na ujasiri kwa wanamichezo wenye ulemavu duniani.

Mbali na kuweka rekodi, safari hiyo inalenga kuchangisha fedha kwa ajili ya mashirika ya Save the Children na Challenged Athletes Foundation.

Kufikia sasa, Lahna amefanikiwa kuchangisha zaidi ya dola 80,000 kati ya lengo lake la dola 250,000 litakalosaidia watoto na wanamichezo wenye ulemavu.

Wadau wa michezo duniani wamepongeza juhudi za Lahna, wakisema safari yake ni ushahidi kuwa dhamira, nidhamu na uvumilivu vinaweza kuvunja mipaka na kuwahamasisha watu wengi zaidi kushiriki katika michezo bila kujali changamoto walizonazo.

Related Articles

Back to top button