Kenya yatoa neno ukarabati uwanja AFCON

NAIROBI: Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mataifa ya Afrika 2027 (AFCON 2027) nchini Kenya, Nicholas Musonye, amesema nchi hiyo inaendelea na maandalizi ya viwanja kwa ajili ya mashindano hayo, licha ya kukiri kuwa ukarabati wa Uwanja wa Moi International Sports Centre (MISC) Kasarani bado unakabiliwa na changamoto.
Kauli ya Musonye imekuja wakati wakaguzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wakitarajiwa kuwasili mwezi ujao nchini Kenya, Tanzania na Uganda ili kutathmini kiwango cha maandalizi ya nchi hizo zitakazoshirikiana kuandaa AFCON 2027.
Mashindano hayo ya mataifa 24 yanatarajiwa kuanza Juni 19 hadi Julai 17, 2027, huku CAF ikisisitiza kuwa viwanja vya mechi na mazoezi vinapaswa kuwa vimekamilika ifikapo Januari 2027.
Ukaguzi wa awali uliofanyika Februari 2026 ulibaini kuwa hakuna hata uwanja mmoja kati ya uliopendekezwa na nchi tatu hizo uliokuwa umefikia viwango vinavyotakiwa na CAF, jambo lililoifanya taasisi hiyo kutoa masharti mapya kuhusu miundombinu, uendeshaji, fedha na utawala wa maandalizi.
Akizungumza na Nation Sport, Musonye alisema Kenya ipo kwenye njia sahihi ya kutimiza masharti hayo kabla ya ukaguzi wa mwezi Agosti.
“Tupo kwenye mstari sahihi. Kufikia wakati wakaguzi wa CAF watakapowasili mwezi ujao, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kuwaonyesha hatua kubwa tulizofikia,” alisema Musonye.
Kenya imepanga kutumia Talanta Sports City yenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 na MISC Kasarani yenye uwezo wa mashabiki 48,000 kama viwanja vikuu vya mashindano hayo.
Kwa mujibu wa CAF, viwanja vinavyotarajiwa kutumika vinapaswa kuwa vimekamilika kwa angalau asilimia 80 kabla ya ukaguzi wa mwezi Agosti. Wakati ujenzi wa Talanta Sports City umeshafikia zaidi ya asilimia 90, ukarabati wa Kasarani bado unaendelea, ukiwemo uwekaji wa nyasi mpya na maboresho mengine muhimu.
Musonye alikiri kuwa Kasarani ndiyo eneo linalompa wasiwasi zaidi, lakini akaeleza kuwa kazi zinaendelea kwa kasi na kwamba maboresho makubwa yanatarajiwa kukamilika kabla ya wakaguzi wa CAF kuwasili.
“Wasiwasi wangu mkubwa kwa sasa ni Kasarani. Hata hivyo, kufikia mwisho wa wiki hii mambo mengi yatakuwa yamekamilika na tunaamini wakaguzi wa CAF wataridhishwa kuwa tunatimiza masharti yao,” alisema.
Ukaguzi ujao wa CAF unatajwa kuwa wa muhimu kwa Kenya, Tanzania na Uganda katika kuthibitisha utayari wao wa kuandaa kwa pamoja fainali za AFCON 2027, mashindano yatakayofanyika kwa mara ya kwanza yakishirikisha mataifa matatu ya Afrika Mashariki.




