Burudani

Wasanii Afrika Mashariki  kuungana kuimarisha sanaa

KENYA: Wasanii wa fani mbalimbali za sanaa katika Ukanda wa Afrika Mashariki wametakiwa kuungana na kuwa na sauti moja ili kuleta mabadiliko chanya na kukuza sekta ya sanaa katika kanda hiyo.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha mada katika kongamano la The East African Art Nexus (TEANEX) lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, Adrian Nyangamale, amesema umoja wa wasanii ni msingi muhimu katika kuimarisha na kutangaza sanaa ya Afrika Mashariki kimataifa.

Amesema kuwa sekta ya sanaa ina wigo mpana, lakini mafanikio yanayoonekana nchini Tanzania, hususan katika muziki, filamu na sanaa za maonyesho, yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano uliopo kati ya serikali na wasanii.

“Serikali imekuwa mstari wa mbele kusaidia wasanii kwa kuanzisha mabaraza na mashirikisho yanayowaunganisha na kuwapa nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya sekta hii,” amesema.

Nyangamale ameongeza kuwa kongamano hilo lina lengo la kuunda jukwaa (platform) la kuwaunganisha wasanii wa Afrika Mashariki ili wawe na sauti ya pamoja katika mchakato wa kuleta mabadiliko na kuongeza utambuzi wao katika ngazi ya kitaifa na kikanda.

Kongamano hilo limewakutanisha wasanii kutoka Tanzania, Kenya na Uganda, ambapo zaidi ya wasanii 30 kutoka Tanzania walishiriki.

Nyangamale ametoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) pamoja na Alliance Française kwa kuwezesha ushiriki wa wasanii katika kongamano hilo.

Kwa upande wake, Msanii Mwangaza Paul amesema kuwa sekta ya filamu nchini Tanzania inaendelea kufanya vizuri, hasa katika eneo la tamthilia ambazo zimefanikiwa kuvutia soko kubwa la watazamaji ndani na nje ya nchi.

Kwa ujumla, wadau wa sanaa wameeleza kuwa ushirikiano na umoja wa wasanii ni nguzo muhimu katika kukuza ubunifu, ajira na mchango wa sanaa katika uchumi wa nchi za Afrika Mashariki.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button