Waamuzi watishia kuisusa Ligue 1

PARIS:CHAMA cha waamuzi nchini Ufaransa kimesema kitawashawishi waamuzi wake kususia kuchezesha michezo ya Ligi kuu nchini humo Ligue 1 kama shirikisho la soka nchini humo halitawahakikishia usalama waamuzi kufuatia kile kinachodaiwa kuwa matamshi ya chuki yaliyotolewa na raia wa klabu ya Olympique Marseille Pablo Longoria.
Longoria alipinga uteuzi wa mwamuzi Jeremy Stinat kuchezesha mchezo wa Olympique Marseille dhidi Auxerre Jumamosi mchezo ambao hata hivyo alichezesha na Marseille walipoteza kwa mabao 3-0.
Baada ya mchezo huo Longoria alidai wamepoteza kwa sababu mwamuzi Stinat amejaa rushwa, matamshi hayo yalipelekea Longoria kufungiwa na bodi inayosimamia Ligue 1 LFP kutohudhuria viwanjani kwa michezo 15 ya ligi hiyo.
Vyombo vya habari nchini Ufaransa vimeripoti kuwa magari mawili ya familia ya Stinat yalitobolewa matairi. Na sasa mwamuzi huyo anajihisi yupo kwenye hatari ya kushambuliwa na mashabiki.
Jopo la waamuzi kutoka katika chama cha waamuzi nchini Ufaransa (SAFE) lilikutana na Waziri wa michezo wa nchi hiyo Marie Barsaq kuelezea masikitiko yao juu ya matukio hayo yanayotishia usalama wa waamuzi na kuchafua taswira ya soka safi la Kifaransa.
Taarifa iliyotolewa na SAFE imesema tayari imemshauri Stinat kuanza mchakato wa kisheria wa kushughulikia usalama wake.