Kumi wanaopewa kipaumbele kumrithi Klopp

MSAKO wa kocha mpya wa Liverpool unaendelea huku wakuu wapya wa soka wa klabu hiyo Michael Edwards na Richard Hughes wakifanyia kazi mpango wa utekelezaji kwa ajili ya msimu mpya.
Januari mwaka huu Jürgen Klopp alitangaza kwamba ataachia ngazi Anfield baada ya miaka tisa ya kuinoa klabu hiyo.
Wafuatao ni makocha kumi wanaopewa kipaumbele kurithi nafasi hiyo.
1. Xabi Alonso (Bayer Leverkusen)
Alonso alikuwa kipaumbele cha kwanza kumrithi Klopp baada ya tangazo lake Januari na mhispania huyo anabaki kuongoza orodha ya wakuu wa Liverpool.
2. Ruben Amorim (Sporting CP)
Licha kuwa na umri wa miaka 39 tu, Amorim ameibuka kuwa mshindani mkubwa kuchukua nafasi ya ukocha Anfield majira yajayo ya kiangazi.
3. Roberto De Zerbi (Brighton)
De Zerbi ni kocha mwingine mwenye faida kubwa ya uzoefu wa Ligi Kuu England katika vita ya kuwania kumrithi Klopp.
4. Julian Nagelsmann (Germany)
Nagelsmann, alikuwa mshindani wa juu wa ukocha wa Tottenham na Chelsea majira yaliyopita ya kiangazi, mkataba wake utakwisha timu ya taifa ya Ujerumani baada ya fainali za Kombe la Ulaya zitakazofanyika Juni hadi Julai, Ujerumani.
5. Thomas Tuchel (Bayern Munich)
Kwa sasa Tuchel amekalia kuti kavu Bayern lakini tayari pande hizo mbili zimetangaza uamuzi wao kufikia makualiano ya kukatisha mkataba majira yajayo ya kiangazi.
6. Unai Emery (Aston Villa)
Uwezekano wa Liverpool kumteua Emery unategemea vita ya Aston Villa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
7. Zinedine Zidane
Hivi karibuni Zidane amekiri angependa kurejea kwenye ukocha baada ya kuondoka Real Madrid mwisho wa 2020-21.
8. Xavi Hernandez (Barcelona)
Xavi alifuata nyayo za Klopp Januari kwa kutangaza kwamba ataachia mikoba ya ukocha Barcelona mwisho wa msimu wa 2023-24.
9. Marco Silva (Fulham)
Kocha wa zamani wa Everton, Silva ni mshangao mwingine katika vita ya kurithi mikoba ya Klopp Anfield.
10. Pep Lijnders (Liverpool)
Chaguo moja ambalo lipo tayari Liverpool ni kocha msadizi wa sasa wa Klopp ingawa Edwards na Hughes wangependa tu kumpa nafasi mdachi huyo iwapo watashindwa kuwateua waliopewa kipaumbele.