Riadha

Usain Bolt amuonya Gout

ATLANTA, Marekani: MKONGWE wa mbio fupi duniani, Usain Bolt, amempa ushauri maalum nyota chipukizi wa Australia, Gout Gout, akimtaka asisahau mchezo wa riadha huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na watu sahihi wa kumsaidia katika safari yake ya kimichezo.

Bolt ametoa ushauri huo wakati mafanikio ya Gout yakiendelea kuvutia dunia, baada ya kutetea taji la mita 200 katika Mashindano ya Riadha ya Australia Aprili 12 kwa muda wa sekunde 19.67, akiibuka na rekodi mpya dhidi ya baadhi ya nyakati bora duniani.

Gout, ambaye ana umri wa miaka 18, aliwashinda wakimbiaji wakubwa akiwemo Mmarekani Erriyon Knighton, huku muda wake ukizidi hata ule wa Bolt akiwa kijana (19.93 aliokimbia mwaka 2004).

Akizungumza na CNN, Bolt amesema mafanikio ya mapema yanaweza kuambatana na changamoto za ushawishi na mizunguko mingi ya maisha ambayo inaweza kumtoa mchezaji kwenye malengo yake ya msingi.

“Katika umri huo mdogo, kama nilivyopitia, unaweza kuanza kuvutwa huku na kule na kusahau riadha. Natumaini ana watu sahihi wanaomwelekeza na kumweka kwenye mstari,” amesema Bolt.

Gout kwa sasa anatarajiwa kufanya kushiriki Diamond League katika mbio za mita 200 mjini Oslo Juni 10, huku pia akitarajiwa kuchagua kuacha Michezo ya Jumuiya ya Madola Glasgow ili kujikita zaidi kwenye Mashindano ya Dunia ya Vijana yatakayofanyika Oregon mwezi Agosti.

Nyota huyo chipukizi anaendelea kuonekana kama moja ya vipaji vipya vinavyoweza kutikisa riadha ya dunia katika miaka ijayo.

Related Articles

Back to top button