Tyson wa Bongo aahidi kipigo kwa Mjuaji
BONDIA Hassan Ndonga ‘Tyson wa Bongo’ ametamba kumpiga mpinzani wake ajaye Tasha Mjuaji katika pambano la usiku wa kisasi la kumsindikiza Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ dhidi ya Erick Katompa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Pambano hilo lisilokuwa la ubingwa linatarajiwa kuchezwa Julai 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO Ndonga amesema kwa mazoezi makali aliyofanya
‘gym’ anaamini kabisa mpinzani wake huyo hatotoka salama na kumtahadharisha kuwa makini.
“Namtahadharisha mpinzani wangu tu kwamba kipigo atakachopata ni cha paka mwizi, hatacheza muda mrefu,” amesema na kuongeza kuwa raundi tatu pekee zinatosha
kumaliza kazi yake.
Katika usiku wa kisasi jumla ya mapambano kumi yanatarajiwa kupigwa na miongoni mwao ni Nassibu Ramadhani dhidi ya Loren Japhet, Ramadhani Iddi kuzichapa na Peter Toshi wa
Mbweni JKT na wengine.




