Burkina Faso, Mali, Niger zajipambania uandaaji Afcon 2032

JOHANNESBURG: Nchi za Burkina Faso, Mali na Niger zimeripotiwa kupiga hatua zaidi kwenye kupigania nafasi ya uaandaaji wa pamoja wa michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2032.
Hiyo ni baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuthibitisha kupokea na kuidhinisha rasmi maombi yao ya awali.
Taarifa iliyotolewa na CAF leo Jumatano imesema hatua hiyo inaziruhusu nchi hizo tatu kuendelea na maandalizi ya zabuni yao ya pamoja ya kuwania uenyeji wa michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka Afrika.
Imeelezwa kuwa, endapo zabuni yao itapitishwa, nchi hizo zitaweka rekodi ya kwa mara ya kwanza mataifa hayo matatu ya Ukanda wa Sahel kuandaa kwa pamoja Afcon.
Imefafanuliwa, serikali na viongozi wa michezo wa nchi hizo wanatazamia mradi huo kama fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuonyesha uthubutu wao wa kuandaa tukio la kiwango cha hadhi ya kimataifa.
Aidha, nchi hizo sasa zitasubiri usahili na tathmini ya kina kutoka CAF juu ya nyaraka za kiufundi watakazowasilisha kwa ajili ya mipango ya miundombinu kabla ya shirikisho hilo kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu mwenyeji wa Afcon 2032.




