Serikali yaahidi kuendelea kuunga mkono watengeneza maudhui mtandaoni

DAR ES SALAAM: Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali itaendelea kuunga mkono watengeneza maudhui bora ya mtandaoni ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya sekta ya ubunifu nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla ya kumkabidhi tuzo mtengeneza maudhui bora wa mtandaoni, Abdul Chacha maarufu Headmaster, iliyotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Msigwa amesema vijana wanapaswa kutumia fursa zilizopo katika uchumi wa kidijitali kujenga ajira na kujiongezea kipato kupitia maudhui yenye tija kwa jamii.
Amesema pamoja na umuhimu wa kutengeneza maudhui, ni lazima yawe yenye ubora na maadili ili yaweze kuelimisha na kuvutia watazamaji.
“Unaweza kutengeneza maudhui ambayo mtu akiyafungua baada ya sekunde mbili anayazima kwa sababu hayana manufaa kwa jamii.
Tunahitaji maudhui yanayojenga na kuelimisha,” amesema Msigwa.
Ameongeza kuwa Serikali tayari imetoa zaidi ya Sh bilioni 14 kupitia mikopo kwa watengeneza maudhui mtandaoni, ambapo zaidi ya wasanii 1,300 wamenufaika na fedha hizo zilizowawezesha kununua vifaa vya kisasa na kuboresha kazi zao.
Katika hafla hiyo, Abdul Chacha alikabidhiwa Sh milioni tano kama tuzo ya kutambua mchango wake katika kutengeneza maudhui ya kuelimisha jamii kupitia mtandao wa YouTube.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, CPA Nyakaho Mahemba, alisema mbali na tuzo ya fedha, Abdul Chacha amepatiwa mafunzo ya kuboresha kazi zake, kuzisajili katika mifumo ya kisasa ya mapato ya kidijitali pamoja na kuunganishwa na mfuko wa hifadhi ya jamii ili kunufaika na mafao ya uzeeni.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Abdul Chacha ameishukuru Serikali na BASATA kwa kutambua kazi yake, akisema hatua hiyo ni motisha kwa watengeneza maudhui wengine kuendelea kuzalisha kazi zenye ubora.
Amewataka wasanii wenye uzoefu kuendelea kuwasaidia na kuwaelekeza vijana wanaoingia kwenye tasnia hiyo, akibainisha kuwa wengi wao hawajapata elimu ya kutosha kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya ubunifu.
Abdul Chacha amesema kabla ya kuingia katika utengenezaji wa maudhui alikuwa akiendesha bodaboda kwa miaka mitano akipambana kutafuta riziki, lakini sasa kazi hiyo imemwezesha kujipatia kipato cha uhakika, kuhudumia familia yake na kutoa ajira kwa wasanii wengine saba wanaofanya kazi pamoja naye.




