Simba yamshusha Bakari Msimu

DAR ES SALAAM: WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamemtambulisha mchezaji mwingine katika nafasi ya kiungo mshambuliaji Bakari Msimu kwa mkataba unaotajwa wa miaka miwili.
Simba ilimtambulisha Msimu, aliyekulia katika akademi ya Coastal Union kuanzia timu ya U17 kabla ya kupanda U20 na baadaye kikosi cha wakubwa msimu wa 2023/24.
Katika misimu yake mitatu akiwa Coastal, Msimu ameendelea kukua na kuendelea kuboreka ambapo msimu wa mwaka jana alipewa unahodha wa kikosi hicho, akimaliza ligi akiwa amefunga mabao manne na kutoa pasi tatu za mabao msimu wa 2024/25.
Mbali na mafanikio yake ngazi ya klabu, Msimu pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Ngorongoro Heroes kilichoandika historia kwa kutwaa ubingwa wa CECAFA U20 baada ya kuichapa Kenya katika mchezo wa fainali.
Simba inaendelea na harakati zake za kutambulisha wachezaji wake kuelekea katika maandalizi ya msimu mpya.
Wekundu hao ni miongoni mwa timu mbili za Tanzania zinazojiandaa na mashindano ya Cecafa yatakayofanyika nchini Rwanda hivi karibuni.




