Trump aikataa filamu inayomuhusu ya ‘The Apprentice’
NEW YORK: TIMU ya wanasheria wa Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump imepiga marufuku filamu ya ‘The Apprentice’ kwa kuiandikia barua ya kusitisha na kuacha kuonyesha filamu hiyo lakini hadi leo hawajasema chochote kuhusu filamu hiyo inayotarajiwa kuachiwa Oktoba 11, 2024 mwezi mmoja kabla ya uchaguzi.
Wanasheria hao waliizuia filamu hiyo katika onyesho la kwanza katika Tamasha la filamu la 77 la Cannes lililofanyika Mei 20, 2024 lakini siku zinavyozidi kukaribia kwa ajili ya uzinduzi wake upande wa Trump bado haujaonyesha nia ya kuruhusu filamu hiyo itolewe.
Filamu hiyo imepangwa kuanza kuonyeshwa nchini Marekani katika majumba ya sinema kupitia kampuni ya Tom Ortenberg’s Briarcliff Entertainment na Rich Spirit.
Msemaji wa kampeni ya Trump, Steven Cheung ameshutumu filamu hiyo katika taarifa yake, ingawa Rais huyo wa zamani wa Marekani hajatoa vitisho vyovyote vya kisheria dhidi ya filamu hiyo.
Alipoulizwa juu ya uwezekano wa vitisho vya Trump siku za usoni katika onyesho la kwanza la huko New York, karibu na Trump Tower, Muongozaji wa filamu hiyo, Ali Abbasi alisimama karibu na sinema yake na kutilia shaka timu ya Trump ingemshtaki.
“Nina shaka watarudi baada ya filamu,” Abbasi aliiambia The Hollywood Reporter. “Sidhani hivyo, kwa sababu wanajua tuko sahihi. Wanajua hakuna cha kutushitaki, tulikuwa makini katika uandishi wa habari na tumefuata sheria zote.”
Katika uzinduzi wa awali ambapo filamu hiyo ilizuiliwa mastaa kadhaa walihudhuria akiwemo Sebastian Stan, Jeremy Strong na Maria Bakalova. Filamu hiyo imeandikwa na Gabriel Sherman imetayarishwa na Daniel Bekerman na mtayarishaji mkuu akiwa Amy Baer.
Mwanasheria wa zamani wa Trump Michael Cohen, ambaye alizungumza na vyombo vya Habari, alisema alikuwa na hamu ya kuona filamu hiyo inayomuhusu Trump kama ambavyo wengi wanatamani kuiona.
Filamu hiyo inaangazia uhusiano kati ya Trump (Stan) na wakala wa nguvu wa New York, Roy Cohn (Strong), wakati Trump alipokuwa Tajiri wa mali zisizohamishika katika miaka ya 1970 na 1980, ikionyesha jinsi Cohn alivyomtengeneza Trump kuwa Trump aliye sasa anayegombea urais wa Marekani kwa mara nyingine.