Afunguka kutokuwa staa kama Shah Rukh Khan

MUMBAI: MUIGIZAJI na mfanyabiashara Akshaye Khanna amesema anaridhika na maisha yake ya sasa licha ya kutokuwa maarufu kama walivyo wasanii wenzake alioanza nao uigizaji akiwemo Shah Rukh Khan, Akshay Kumar, Aamir Khan na Salman Khan.
Akshaye amesema yeye na wasanii hao walianza kazi zao za uigizaji katika filamu mbalimbali kwa wakati mmoja lakini wenzake wote wamekuwa maarufu mno kuliko yeye jambo linalowashangaza wengi wakidhani amebaniwa.
Katika mahojiano na Anurradha Prasad, Akshaye amefafanua sababu iliyomfanya kutokuwa maarufu na staa licha ya kutamba na filamu ya ‘Dil Chahta Hai’, ‘Border’, ‘Taal’ akidai alikosa muda wa kutangaza kazi zake kwa kuwa muda mwingi alikuwa akiuwekeza katika biashara zake ili awe tajiri mkubwa kupitia biashara tofauti na filamu:
“Kama muigizaji, ili filamu zako ziwe maarufu unahitaji kuhudhuria matamasha ya Gadar, Dilwale na kila sherehe, kufanya mahojiano mengi au kutengeneza mijadala mbalimbali ili uzungumzwe lakini mimi nilikuwa tofauti sikuwa na muda wa kufanya hayo yote niliamini katika ubora wa filamu zangu na biashara ninazofanya.
“Fikiria mimi ni mfanyabiashara, na nina biashara yenye thamani ya crore 500 Sasa, nina ndoto ya kuwa kama tajiri mkubwa Ratan Tata au Dhirubhai Ambani, sasa kwa hapo kweli sina mafanikio ya Shah Rukh Khan?”
Hata hivyo Akshaye Khanna amefafanua zaidi kuwa katika nchi yenye zaidi ya watu milioni 120, ni watu wapatao 15 hadi 20 pekee waliobahatika kuwa waigizaji wakubwa amuwezi kuwa wote.
Akshaye hivi karibuni ameonekana katika filamu inayomuonyesha kama Mfalme Aurangzeb katika filamu ya Chhaava, Filamu ya matukio ya kihistoria, iliyotokana na maisha ya Chhatrapati Sambhaji Maharaj.
Pia Akshaye ataonekana katika filamu ya ‘Dhurandhar’, ikiongozwa na Aditya Dhar. Filamu hiyo pia ina nyota Ranveer Singh, Sanjay Dutt na wengine wengi.