Trent atenga kibunda kuinunua Nantes
LIVERPOOL, ENGLAND: Beki wa Liverpool,r Trent Alexander-Arnold anatazamiwa kuwa mmiliki mpya wa klabu ya FC Nantes inayoshiriki Ligi kuu ya Ufaransa, Ligue 1 katika hatua ambayo imeshitua wadau wa soka duniani.
Beki huyo wa kimataifa wa Uingereza amekuwa akihusishwa na kuondoka Anfield msimu ujao baada ya mkataba wake kumalizika.
Kumekuwa na uvumi wa kitasa hicho cha Arne Slot kuhamia kwa miamba ya La Liga Real Madrid kwa uhamisho wa bure lakini inaonekana kama Alexander-Arnold anaweza kuwa na timu yake binafsi hivi karibuni.
Gazeti la Ufaransa L’Equipe linadai kwamba Alexander-Arnold yuko tayari kutoa ofa ya Euro milioni 100 ili kuwa mmiliki wa FC Nantes ya nchini Ufaransa kupitia mfuko mmoja wa uwekezaji wa nchini England unaosimamiwa na baba yake mzazi.
Gazeti hilo linadai Kylian Mbappe ‘anawahamasisha’ wanasoka wengine kuchukua hatua katika umiliki wa klabu baada ya mshambuliaji huyo wa Real Madrid hivi majuzi kununua asilimia 80 ya klabu ya Ligue 2 nchini humo Stade Malherbe Caen.
Mfanyabiashara Mfaransa, Waldemar Kita, ambaye amekuwa akimiliki Nantes tangu 2007, inaonekana amechoshwa na matatizo ya kimichezo na kifedha yanayokabili eneo la pwani ya magharibi mwa Ufaransa la Loire-Atlantique.