Filamu

Idris Elba kujenga studio ya filamu Zanzibar

 

MSANII nguli kutoka Hollywood Marekani, Idris Elba anatarajiwa kujenga studio kubwa ya kuandalia filamu za kimataifa eneo la Fumba visiwani Zanzibar.

Waziri wa Uwekezaji wa Zanzibar Sharif Ali Sharif amesema muigizaji huyo amepewa eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 80 eneo la Fumba ili kukuza filamu zinazozalishwa nchini kufikia viwango vya kimataifa.

Waziri Sharif amesema hayo katika ufunguzi wa Tamasha la 27 la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) linaloendelea katika eneo la Mji Mkongwe kwa kuonyesha filamu 70 zilizopitishwa kugombea tuzo mbalimbali katika tamasha hilo.

Waziri Sharif amesema muigizaji na mzarishaji wa filamu huyo Idris Elba, atakuja kuwekeza Zanzibar kwa sababu ya hamasa kubwa iliyotokana na ukuaji wa filamu nchini ambazo zimekuwa zikitiliwa mkazo mkubwa na Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF).

Katika hatua nyingine Waziri Sharif ameutaka uongozi wa ZIFF kuweka programu endelevu baada ya kukamilika kwa tamasha hilo kila mwaka ili kuwezesha waandaaji filamu wapya kuwa na utaalamu wa uandaaji filamu wenye kiwango cha kimataifa.

¨Baada ya tamasha hili kukamilika, nawaomba uongozi wa ZIFF uendelee kuweka mikakati ya kusaidia watengeneza filamu kupata elimu ya filamu ili waweze kufikia kiwango cha kimataifa katika soko la kimataifa,¨ amesema Waziri Sharif.

Related Articles

Back to top button