Tanzania yaitaka BAFCON
KIKOSI cha timu ya taifa ya soka la ufukweni, kimewasili salama nchini Misri na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye Fainali za Afrika Soka la Ufukweni (BAFCON 2024).
Timu hiyo iliondoka jana kuelekea nchini Misri katika mashindano yanayoanza kutimu vumbi Jumamosi Oktoba 19 hadi 26, katika fukwe za Hunghada nchini Misri.
Tanzania inashuka dimbani kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Morocco Oktoba 19, itakuwa mwakilishi pekee kutoka ukanda wa CECAFA huku ikiwa kundi A na Morocco, Misri na Ghana.
Kocha mkuu wa Tanzania Jaruph Juma amesema wamefika salama na wachezaji wapo tayari kupambania taifa katika michuano hiyo na wanahitaji kuanza vizuri katika mchezo wa kwanza dhidi ya Morocco.
“Tulifanya maandalizi ya kutosha tukiwa nyumbani, tupo tayari kikubwa tunasubiri siku ya mechi, mechi yetu na Morocco ni muhimu sana kwani inatupa taswira ya wapi tunapokwenda katika mashindano haya,” amesema Jaruph.
Mbali na mashindano hayo ya bara, Mataifa yote yatakuwa yakitafuta nafasi ya kucheza fainali ya kombe la Dunia mwaka 2025, inayotarajiwa kufanyika barani Afrika kwa mara ya kwanza, Shelisheli itakuwa wenyeji wa michuano hiyo.