Soka La Ufukweni

JWTZ yataka timu za jeshi soka la ufukweni

DAR ES SALAAM: Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) Brigedia Jenerali Simon Pigapiga amewataka wahitimu wa mafunzo ya soka la ufukweni ambao ni maofisa wa Jeshi kuanzisha timu za Jeshi za mchezo huo zitakazoleta ushindani nchini.

Hayo ameyasema Dar es Salaam leo kwa niaba ya Mkuu wa Utawala na Rasilimali watu Jeshini Meja Jenerali Michael Gaguti, katika hafla ya kufunga mafunzo ya siku 10 kwa wahitimu 24 walioshiriki mafunzo hayo.

Amesema soka la ufukweni ni fursa kwa vijana mbali na kukuza vipaji ni ajira, husaidia kukuza utalii wa ndani kupitia mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa hivyo kuwaomba watambue jukumu lao la kuwa mabalozi wa mchezo huo nchini na pengine popote duniani.

“Endeleeni kueneza mafunzo haya mliyoyapata kwa askari wenzenu maana ninyi nimeambiwa ni makocha mnaenda kufundisha tunataka tuone matunda, mfundishe, msiishie kucheza bila kuanzisha timu kutoka maeneo mbalimbali ya vikosi vya Jeshi,”amesema.

Amesema: “Tunategemea kwa muda mfupi tutapata timu nyingi sana, sio maeneo yenye bahari tu bali sehemu zote zenye maziwa, tunategemea timu ziibuke huko,”.

Amesema Mkuu wa Majeshi Jenerali Jacob Mkunda ametoa pongezi kwa washiriki wote wa kozi walioanza na kumaliza kozi hiyo kwa mafanikio makubwa.

Mbali na hayo, amewataka wahitimu kujiendeleza zaidi katika mchezo huo kwani mchezo wa soka la ufukweni hauhitaji tu ujuzi bali nidhamu ya mwili, mbinu maalum na uelewa wa mazingira ya kipekee ya Uwanja wa mchanga.

Amesema Jeshi la wananchi wa Tanzania wataendelea kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wadau mbalimbali kuhakikisha mchezo huo unapata msukumo na maendeleo zaidi.

Brigedia Jenerali Pigapiga ameongeza kuwa watatoa ushirikiano kwa kadiri itakavyowezekana kuweka mazingira bora ya mchezo huu wa soka la ufukweni. Pia, kujenga miundombinu ya viwanja kama kiwanja kilichopo Mbweni Ndege beach ambacho kiko katika hatua nzuri za kukamilishwa.

Kwa upande wake, Rais wa TFF Wallace Karia amesema wamefanya utafiti wamegundua wenzao wengi wanatumia askari wa Jeshi ndio maana wakawiwa kumuomba Mkuu wa Majeshi washirikiane.

Amesema mafunzo hayo ni mwanzo tu, watafanya nyingine na kuita mkufunzi wa kimataifa Twalib Bilal ambaye ni Mtanzania lakini ni mkufunzi wa Bara la Asia kuja kuwanoa zaidi.

TFF kwa kushirikiana na JWTZ limeratibu mafunzo hayo ikiwa ni kutimiza azma za maagizo ya Mkuu wa Majeshi Jenerali Jacob Mkunda katika kuhakikisha Jeshi linakua kinara wa kushiriki michezo kitaifa na kimataifa.

Related Articles

Back to top button