Championship yabustiwa zaidi

KAMPUNI ya Startimes imesema itaendelea kuunga mkono Ligi ya Championship ili kuwapa nafasi vijana kuonesha vipaji na kujiuza kimataifa.
Pia, kampuni hiyo imesema inatarajia kuonesha Ligi kubwa za Ulaya zikiwemo La Liga ya Hispania, Ujerumani Bundesliga, Saudi Arabia, Carabao Cup na Copa Del Rey.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Masoko na Maudhui wa Startimes, David Malisa, kwenye uzinduzi wa kampeni mpya ya Zote ndani.
“Ligi zote kubwa zitakuwa Startimes, tunaanza nyumbani na Championship kisha kimataifa na hiyo yote tunataka mashabiki wetu waendelee kubaki na sisi kwa kulipia vifurushi kwa bei ndogo na kuona namna vijana mbalimbali wanavyofanya vizuri,”amesema Malisa.
Meneja wa vipindi na Maudhui kutoka Tv3 Emmanuel Sikawa amesema michuano hiyo yote itaruka kupitia Tv3 na kuhimiza mashabiki wa soka na wadau mbalimbali kutobaki nyuma, na wafahamu kuwa ni wakati sahihi kuona vipaji vya soka vya ndani na kimatifa.
Amesema wamekuwa wakifanya vizuri kuonesha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu kwa silimia 75. Pia, wamekuwa wakionesha michuano tofauti ya Afrika na lengo ni kuhakikisha watu wanapata burudani na kujifunza namna wengine wanavyofanya.
“Tunajua kuwa mashabiki wengi wanapenda mpira na awamu hii tutakuwa tunachambua, tutawafuata mashabiki mahali walipo kuona wananufaika vipi na michezo hii,” amesema Sikawa.
Pia ameeleza kuwa, Startimes kwa kushirikiana na Tv3 sio tu wanatoa fursa kwa mashabiki wa soka kufurahia bali ajira kwa wadau na wachambuzi kwa ajili ya kuchambua michezo hiyo mikubwa ya kimataifa.