Barker: Simba yaanza kutafuta wachezaji wapya

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema benchi la ufundi tayari limeanza kazi ya kutafuta wachezaji wa kuongeza nguvu kikosini kuelekea msimu ujao licha ya kuridhishwa na ubora wa kikosi cha sasa.
Barker amesema mchakato huo ni sehemu ya mipango ya kuhakikisha timu inaendelea kuwa na ushindani mkubwa katika mashindano ya ndani na ya kimataifa, huku akisisitiza kuwa kwa sasa bado wanafanya tathmini ya maeneo yanayohitaji kuimarishwa.
Katika mahojiano maalum yaliyofanyika Dar es Salaam amesema kwa sasa Simba ina kikosi kizuri na chenye ushindani, lakini kama ilivyo kwa klabu kubwa, ni muhimu kuendelea kufanya maboresho ili kukidhi mahitaji ya timu kila msimu.
“Tumeshanza kufanya kazi ya usajili, lakini siwezi kuzungumzia majina ya wachezaji tunaowafuatilia kwa sasa. Huo ni mchakato unaoendelea,” amesema Barker.
Kocha huyo pia alieleza kufurahishwa na mafanikio ya usajili uliofanywa katika dirisha dogo la Januari, akisema wachezaji walioletwa kipindi hicho wameendelea kuwa sehemu muhimu ya kikosi na wametoa mchango mkubwa katika safari ya timu msimu huu.
Amebainisha kuwa ushindani wa ligi umekuwa mkubwa na kila timu imeonesha dhamira ya kupata matokeo, jambo ambalo limeifanya Simba kuendelea kupambana kwa nguvu katika kila mchezo.
Akizungumzia mashindano ya kimataifa, Barker amesema Simba bado ina hamu ya kuendelea kufanya vizuri na kushindana katika kiwango cha juu zaidi, akieleza kuwa mafanikio ya timu katika michuano hiyo ni moja ya malengo makubwa ya klabu.
Kocha huyo hakuficha hisia zake kuhusu mechi za dabi, akisema matokeo ya baadhi ya michezo hiyo yaliwaumiza wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki kutokana na matarajio makubwa yaliyokuwepo.
“Mechi za dabi zina hisia za kipekee. Tunafahamu namna mashabiki wanavyozipokea na jinsi wanavyotaka kuona timu ikishinda. Wakati mwingine matokeo yanapokuwa tofauti na matarajio, maumivu yanakuwa makubwa kwa kila mmoja,” amesema.
Ametoa shukrani kwa mashabiki wa Simba kwa kuendelea kuiunga mkono timu katika nyakati zote, akisisitiza kuwa sapoti yao imekuwa chachu ya wachezaji kupambana na kutafuta mafanikio makubwa zaidi.
Barker amesema Simba itaendelea kujijenga na kufanya maboresho yatakayoiwezesha kubaki katika ushindani wa juu huku ikilenga kutwaa mataji na kuandika historia zaidi katika soka la Afrika.




