Simba , Yanga ni kisasi au dozi Kombe la Muungano Zanzibar

ZANZIBAR:MIAMBA ya soka Tanzania, Simba na Yanga leo zinatarajiwa kumenyana katika mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano utakaopigwa saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, huku ikiwa ni lazima mshindi apatikane ili kubeba taji hilo, hali inayotabiri pambano la nguvu na presha kubwa kwa timu zote mbili.
Timu zote zimeingia fainali zikiwa katika kiwango bora, si tu kwenye michuano hiyo bali pia katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba ilitinga hatua hiyo baada ya kuifunga Mafunzo bao 1-0 katika robo fainali kabla ya kuitandika Mlandege mabao 3-0 kwenye nusu fainali.
Kwa upande wa Yanga, ilionesha ubora wake kwa kuichapa Muembe Makumbi City mabao 4-0 kwenye robo fainali na kisha kuiondoa Azam FC kwa ushindi wa mabao 2-1.
Mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube, amekuwa moto wa kuotea mbali baada ya kufunga mabao matatu katika michuano hiyo. Aidha, Yanga inajivunia uwepo wa nyota wengine kama Allan Okello, Max Nzengeli na Duke Abuya, huku safu ya ulinzi ikiongozwa na Ibrahim Bacca.
Kwa upande wa Simba, mshambuliaji Seleman Mwalimu ameonesha makali kwa kufunga mabao mawili, akisaidiwa na wachezaji kama Clatous Chama, Yusuph Kagoma, Rushine De Truck na Nuckson Kibabage ambao wamekuwa katika kiwango kizuri.
Katika rekodi za michuano hiyo, Yanga inaingia uwanjani ikisaka taji la nane, ikiwa mara ya mwisho ilitwaa mwaka 2025, wakati Simba inalenga ubingwa wake wa saba, ikiwa ilitwaa mara ya mwisho mwaka 2024.
Mshindi wa fainali hiyo ataondoka na kitita cha shilingi milioni 150, huku mshindi wa pili akipata shilingi milioni 100.
Takwimu zinaonesha Yanga imekuwa na ubabe katika mechi za hivi karibuni, baada ya kuifunga Simba mara sita mfululizo, huku mchezo wao wa mwisho wa ligi ukimalizika kwa sare. Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga ilikuwa mwaka 2023 kwenye Ngao ya Jamii kwa penalti 3-1.
Mwamuzi wa pambano hilo atakuwa Dickens Mimisa Nyagrowa kutoka Kenya, akisaidiwa na Ali Mbwana na Yusuph Shombe kutoka Zanzibar, huku mwamuzi wa akiba akiwa Is-haka Mwalile.
Kwa mazingira hayo, macho na masikio ya mashabiki wa soka nchini na visiwani Zanzibar yatakuwa New Amaan Complex kusubiri kuona nani ataibuka bingwa wa Kombe la Muungano mwaka huu huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi.




