Simba yalenga kugeuza historia dhidi ya Al Masry

DAR ES SALAAM: KATIKA hekaheka za kusaka nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids, ameweka bayana dhamira ya kikosi chake kuandika ukurasa mpya kwa kugeuza matokeo dhidi ya Al Masry kutoka Misri.
Mchezo huu wa marudiano wa robo fainali utafanyika kesho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Simba wanahitaji ushindi wa mabao 3-0 ili kufuzu hatua ya nusu fainali, baada ya kupoteza mzunguko wa kwanza ugenini.
Akizungumza kwa kujiamini, Davids amesema kikosi chake kipo tayari kwa vita hiyo muhimu, akisisitiza kuwa safari bado haijafika mwisho na matumaini ya kusonga mbele bado yapo hai.
“Hatujamaliza bado na tunaamini tutacheza vizuri kesho. Tunahitaji mashabiki wetu waendelee kutuamini, tunawahitaji wawe nyuma yetu kwa dakika zote 90,” amesema kocha huyo.
Ameongeza kuwa ushindi huo utatokana na utekelezaji wa mbinu walizojiandalia kwa umakini mkubwa, huku akiamini kwamba wakitimiza hilo, basi nafasi ya kusonga mbele ipo wazi kabisa.
Kwa upande wa wachezaji, Nahodha wa Simba, Mohammed Hussein maarufu kama “Zimbwe Jr”, amesisitiza kuwa maandalizi ya mchezo huo yamekamilika kwa asilimia mia moja na kila mchezaji yupo tayari kwa vita ya kusaka ushindi mkubwa.
“Ugumu upo, lakini tunatambua wajibu wetu. Tunaenda kufanya kazi na kulipa imani ya mashabiki wetu kupitia kauli mbiu yao ya ‘Hii tunavuka na tunavuka kweli’,” amesema kwa msisitizo.
Zimbwe Jr. alifunga kwa kusema kuwa lengo la timu si tu kujivunia kufika robo fainali, bali kuvuka hatua hiyo na kuandika historia kwa kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo ya kimataifa.
Mashabiki wa Simba sasa wana kila sababu ya kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao, huku matumaini ya ushindi mkubwa na kugeuza matokeo yakiwa yamejengwa ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.