Simba Queens waipania JKT Queens

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa Simba Queens umetangaza kuwa mchezo wao dhidi ya JKT Queens utakuwa kama fainali kwao katika harakati za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara.
Hii ni baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Yanga Princess kwa bao 1-0 katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, hali iliyowafanya kuwa matatani kupoteza uongozi wa ligi.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa matokeo hayo yamewapa JKT Queens nafasi ya kuwa mbele, lakini bado Simba Queens hawajakata tamaa.
“Kabla ya mechi na Yanga Princess tulikuwa tunaongoza ligi kwa alama mbili. Yanga hatuna shida naye kwa kuwa tumemuacha kwa tofauti ya alama saba. Sasa tunageukia JKT Queens kwa sababu huu ni mchezo wa fainali kwetu, tunahitaji ushindi,” amesema.
Kuhusu mchezo uliopita, Ahmed amesema wachezaji walipoteza nafasi nyingi za kufunga na kuruhusu bao dakika za mwisho, jambo ambalo halipaswi kujirudia katika mechi inayofuata.
“Mechi ijayo dhidi ya JKT Queens tunatakiwa kuwa makini ili tusifanye makosa ambayo yatatugharimu na kushindwa kufikia malengo yetu ya kutwaa ubingwa wa ligi,” ameongeza.
Mchezo dhidi ya JKT Queens sasa unakuwa wa kuamua hatima ya Simba Queens katika mbio za ubingwa, huku uongozi na wachezaji wakihimizwa kupambana kwa hali na mali ili kurejesha matumaini yao ya kutwaa taji.