Nyumbani

Simba Kumjua Mpinzani wa Robo Fainali CAF Alhamisi

DAR ES SALAAM: KLABU ya Simba, ambayo ni mwakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, inatarajia kumjua mpinzani wake wa robo fainali Alhamisi, Februari 20, 2025. Droo hiyo itafanyika jijini Doha, Qatar.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilitangaza tarehe hiyo hivi karibuni, ambapo pia droo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itapangwa. Tanzania haina mwakilishi katika hatua hiyo baada ya Yanga kutolewa kwenye hatua ya makundi.

Timu nane zilizofuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF ni Simba SC kutoka Tanzania, Zamalek SC na Al Masry za Misri, ASEC Mimosas kutoka Ivory Coast, CS Constantine na USM Alger za Algeria, RS Berkane ya Morocco, pamoja na Stellenbosch FC kutoka Afrika Kusini.

Michezo ya robo fainali ya michuano hiyo miwili itachezwa kwa mikondo miwili. Mechi za kwanza za Ligi ya Mabingwa Afrika zitachezwa kati ya Aprili 1-2, huku marudiano yakifanyika Aprili 8-9, 2025. Kwa upande wa Kombe la Shirikisho, robo fainali ya kwanza itachezwa Aprili 2 na marudiano kufanyika Aprili 9, 2025.

Simba imetinga robo fainali baada ya kumaliza hatua ya makundi ikiwa na alama 12, sawa na CS Constantine. Bravos de Maquis ilimaliza na pointi tano, huku CS Sfaxien ikishika mkia bila pointi yoyote.

Baada ya droo hiyo, Simba itamfahamu mpinzani wake rasmi katika hatua hii muhimu ya michuano.

Related Articles

Back to top button