Ligi Kuu

Simba, JKT mechi ya jasho kusaka pointi tatu

DAR ES SALAAM: KLABU ya Simba SC leo inatarajia kushuka dimbani kuikabili JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Jenerali Isamuhyo, huku ikiwa na lengo la kuendelea kusalia kwenye mbio za ubingwa.

Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kwa pointi 43 baada ya kucheza michezo 20, huku wapinzani wao JKT Tanzania wakishika nafasi ya tano wakiwa na pointi 32 katika idadi sawa ya michezo.

Ushindani wa nafasi za juu unaifanya mechi hiyo kuwa na uzito mkubwa kwa pande zote mbili.

Licha ya ubora wa Simba, wanakutana na JKT Tanzania ambao wamekuwa wakionesha uimara mkubwa, hususan katika safu ya ulinzi, jambo linalowafanya kuwa wapinzani wasiofungika kirahisi. Hali hiyo inalazimisha Simba kupambana kwa nguvu zote ili kuhakikisha wanapata ushindi muhimu.

Akizungumza kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Steven Barker, amesema anatambua ugumu wa mpambano huo lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo chanya.

“Tunaenda kucheza na moja ya timu bora kwenye ligi yenye wachezaji wazuri. Hautakuwa mchezo rahisi kwetu, ila tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Barker.

Kwa upande wa JKT Tanzania, Kocha Ahmad Ally ameweka wazi dhamira ya timu yake kutaka kulipiza kisasi kufuatia kupoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Novemba mwaka jana ambapo walifungwa mabao 2-1 wakiwa nyumbani.

Aidha, JKT Tanzania inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na presha ya kuvunja rekodi mbaya dhidi ya Simba, baada ya kushindwa kupata ushindi katika mechi saba zilizopita walizokutana.

Kwa muktadha huo, mchezo wa leo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, kila timu ikisaka pointi tatu muhimu kwa malengo tofauti,Simba ikiwania ubingwa na JKT Tanzania ikisaka kujiimarisha zaidi kwenye nafasi za juu za msimamo wa ligi.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button