Ligi Kuu

Barker akoshwa ubora wa kikosi kuelekea Simba Day

DAR ES SALAAM: KOCHA wa Simba SC Steven Barker amesema ameridhishwa na maendeleo ya kikosi chake katika kipindi cha maandalizi ya msimu mpya, akieleza kuwa timu imeonesha hatua nzuri tangu ilipoanza kambi nchini Rwanda.

Kocha huyo amesema mechi walizocheza zimewasaidia kuongeza uwezo wa timu kucheza kwa dakika zote 90, huku akibainisha kuwa bado kuna maeneo yanahitaji maboresho kabla ya kuanza kwa changamoto kubwa za msimu.

“Naona tumepiga hatua tangu tulipofika Rwanda. Kila mchezo tumekuwa tukiongeza kiwango na wachezaji wapya wanaendelea kuingia vizuri kwenye mfumo wa timu,” amesema.

Amesema moja ya changamoto iliyopo ni kuwajenga wachezaji katika utimamu wa kucheza muda wote wa mchezo, hasa kutokana na mapumziko mafupi waliyokuwa nayo kabla ya kuanza maandalizi.

“Hatukuwa na muda mrefu wa mapumziko, hivyo mwanzo haukuwa rahisi katika kuwahudumia na kuwasimamia wachezaji, lakini kila siku tunazidi kuwa bora,” ameongeza.

Simba SC inaendelea na maandalizi kuelekea tamasha la Simba Day kabla ya kuanza maandalizi ya mchezo mkubwa dhidi ya Yanga SC wiki ijayo.

Wekundu hao wamerejea Dar es Salaam kujiandaa na tamasha la Simba litakalofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button