Serikali yasistiza wajibu wa kisheria kulipa mirabaha

DAR ES SALAAM: SERIKALI imesisitiza kuwa ulipaji wa mirabaha kwa matumizi ya kazi za ubunifu, ikiwemo muziki, si hiari bali ni wajibu wa kisheria, na imewataka watumiaji wote wa kazi hizo nchini kuzingatia sheria kikamilifu.
Kauli hiyo imetolewa leo Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Emmanuel Ishengoma, kwenye semina ya kutoa elimu ya umuhimu wa ulipaji mirabaha kwa kazi za muziki iliyoandaliwa na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota) kwa kushirikiana na Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa na SOMA.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, Ishengoma amesema kuwa matumizi ya kazi za ubunifu yanapaswa kuendana na sheria bila kulazimishwa, bali kwa uwajibikaji wa hiari kutoka kwa watumiaji.
“Huu ni wajibu wa kisheria, si jambo la maombi wala majadiliano. Kila anayatumia kazi za ubunifu lazima azingatie sheria. Hatutumii nguvu au vitisho, bali tunahimiza uelewa na uwajibikaji,” amesema Ishengoma.
Alieleza kuwa taasisi na wafanyabiashara wanaotumia muziki katika shughuli zao, wakiwemo wa sekta za usafirishaji, hoteli, migahawa na burudani, wanapaswa kujumuisha malipo ya mirabaha kama sehemu ya gharama za kawaida za uendeshaji, sawa na bili za umeme na maji.
Serikali pia imeeleza umuhimu wa kuimarisha taasisi na mashirika ya usimamizi wa pamoja (CMOs) yanayokusanya na kugawa mirabaha, ili yafanye kazi kwa uadilifu, uwazi na uwajibikaji, kuhakikisha mapato yanawafikia wahusika halali.
Ameonya kuhusu changamoto za kiutendaji na kusisitiza haja ya kuendelea kufanya maboresho katika sekta za ubunifu, ikiwemo muziki, filamu na uchapishaji, ili kuboresha uzalishaji, usambazaji na uoneshaji wa kazi hizo.
Kaimu Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki katika Shirika la Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Naomi Mungure, amesema kikao hicho ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uelewa na utekelezaji wa sheria ya hakimiliki.
Amesema kuwa COSOTA inafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki (Sura ya 218 iliyofanyiwa marekebisho), inayolenga kulinda na kuendeleza maslahi ya wamiliki wa hakimiliki, ikiwemo kuhakikisha wanapata malipo stahiki kwa matumizi ya kazi zao katika maeneo ya biashara na umma.
Ameeleza kuwa kumekuwapo mafanikio kufuatia maboresho yaliyoruhusu kuanzishwa kwa mashirika ya usimamizi wa pamoja, likiwemo Society of Music and Advocacy (SOMA) kwa haki za muziki na Tanzania Reproduction Rights Society Limited (TANRRS) kwa kazi za maandishi.
Mungure alisisitiza kuwa kuimarisha utii wa sheria ni muhimu katika kulinda haki za wasanii, kuendeleza uchumi wa ubunifu na kuhakikisha mgawanyo wa faida unakuwa wa haki kwa wadau wote wa sekta hiyo.




