Selena Gomez ala dodo la uongozaji filamu Hollywood

LOS ANGELES, Marekani: Msanii maarufu wa muziki na filamu, Selena Gomez, ameendelea kupiga hatua kubwa katika tasnia ya burudani ya Hollywood baada ya kupata nafasi muhimu zaidi katika kazi yake ya uigizaji na utayarishaji wa filamu.
Taarifa zilizotolewa na kampuni ya Disney zinaeleza kuwa Gomez atafanya kwa mara ya kwanza kazi ya uongozaji wa filamu katika sehemu ya mwisho ya mfululizo wa televisheni wa ‘Wizards Beyond Waverly Place’, hatua inayotajwa kuwa mafanikio makubwa katika safari yake ya kisanii.
Mbali na kuonekana kama muigizaji, Gomez ambaye pia ni mtayarishaji wa vipindi vya televisheni, atakuwa nyuma ya kamera kusimamia utengenezaji wa sehemu muhimu ya mfululizo huo, jambo linaloonesha jinsi anavyozidi kuaminiwa na wadau wa sekta ya filamu nchini Marekani.
Hatua hiyo imekuja wakati ambapo nyota huyo anaendelea kung’ara kupitia mfululizo maarufu wa televisheni wa ‘Only Murders in the Building’, ambao umemletea sifa na uteuzi katika tuzo mbalimbali za kimataifa. Pia anatarajiwa kurejea katika msimu wa sita wa mfululizo huo unaoendelea kurekodiwa nchini Uingereza.
Wachambuzi wa masuala ya burudani wameeleza kuwa hatua ya Gomez kupewa jukumu la uongozaji ni ishara kuwa amefikia kiwango kipya katika Hollywood, akitoka kuwa mwigizaji na mwimbaji maarufu hadi kuwa mmoja wa wanawake wenye ushawishi mkubwa katika uzalishaji wa maudhui ya televisheni na filamu.




