Mume wa Zari, Shakib aomba radhi kuhusu video tata

AFRIKA KUSINI: Bondia wa Uganda, Shakib Lutaaya, ameomba radhi hadharani kwa mke wake, Zari Hassan, baada ya video iliyosambaa mitandaoni kuzua utata na madai ya usaliti.
Akizungumzia msukosuko huo, Shakib alichapisha video mitandaoni akieleza majuto yake na kufafanua msimamo wake.
“Mimi na huyo mtu hatuchumbiani, namjua tu,” alisema. “Niko hapa kuomba msamaha hadharani kwa sababu kosa langu lilijitokeza hadharani. Haikuwa nia yangu kumvunjia heshima mke wangu, familia yangu, au marafiki zangu.”
Klipu hiyo, ambayo tarehe yake haijulikani, iliibuka hivi karibuni mitandaoni ikimuonesha Shakib katika mazingira ya utata na mwanamke asiyejulikana. Ingawa walionekana wakibadilishana ishara za ukaribu na kushikana mikono, wengi walihisi kuwa mwingiliano huo ulikuwa wa kimapenzi, hivyo kuzua uvumi kuhusu matatizo kwenye ndoa yake.
Akijibu sintofahamu hiyo, Zari alichapisha ujumbe mitandaoni akieleza namna wanaume wanavyowanyanyasa wapenzi wao. Akiwa mwenye huzuni, alisisitiza kuwa kwa sasa anajikita katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Wanaume watakuacha jangwani bila maji,” aliandika.
Wanandoa hao hivi karibuni walionekana kwenye kipindi cha uhalisia cha Netflix Young, Famous & African.