Sean ‘Diddy’ Combs amtumia ujumbe mwanae akiwa gerezani
NEW YORK:RAPA Sean Combs maarufu P. Diddy ambaye yupo gerezani akisubiri kesi yake ya ulanguzi wa ngono, ulaghai na usafirishaji haramu kusikikizwa mwakani mwezi Mei,ameelezwa kutuma ujumbe kwa binti yake kwa mara ya kwanza tangu kukamatwa kwake.
Katika ukurasa wake wa Instagram Diddy amemtakia bintiye Love siku njema ya kuzaliwa kwake.
Aliandika, “Happy Birthday to you! Happy Birthday to you! ‘Happy Birthday baby Love! Happy Birthday to you!! Happy Birthday @loveseancombs daddy loves you.”
Kando na maelezo, alichapisha picha za bintiye akila keki iliyovunjika. Combs, 54, ameshiriki kumtakia mtoto huyo siku njema ya kuzaliwa Pamoja na mpenzi wake wa zamani Dana Tran, 30.
Combs alikamatwa na kushitakiwa mwezi uliopita na amekana mashtaka yote. Alinyimwa dhamana na alipoteza rufaa yake ya kupinga uamuzi huo, ikimaanisha kuwa atasalia gerezani hadi kesi yake itakaposikilizwa mwakani.
Katika kituo cha Metropolitan Detention Center huko Sunset, Brooklyn, mawakili wa nyota huyo wameomba ahamishwe baada ya wakili wake Andrew Dalack kudai kituo hicho kina msongamano mkubwa na kisicho na wafanyikazi.
Siku ya Jumatatu iliyopita, ilitangazwa Combs anashitakiwa na watu sita zaidi. Hawa ni pamoja na wanawake wawili wanaodai kuwa aliwabaka, wanaume watatu wanaodai aliwanyanyasa kingono na mvulana mwenye miaka 16 anayedai kuwa alinajisiwa na rapa huyo kwenye tafrija.