Sean Andrew Kibaki akosoa Jumba la rapa Khaligraph
NAIROBI:LICHA ya jumba la rapa kutoka Kenya, Khaligraph Jones kuzungumziwa mno mitandaoni, Mtayarishaji wa Maudhui maarufu wa Kenya Sean Andrew ambaye ni mjukuu wa aliyekuwa rais wa Kenya hayati Emillio Mwai Kibaki, Sean Andrew Kibaki ameibuka na kukosoa baadhi ya maeneo katika jumba hilo akidai halikupata ushauri mzuri wa ujengaji wake.
Sean Kibaki anayejishughulisha na utayarishaji wa maudhui mtandaoni amesema licha ya jumba hilo kupendeza kwa dari zake za juu, nguzo za glasi, na nafasi ya wazi zinazokaribisha wingi wa mwanga wa asili kutoka nje lakini jumba hilo lina mapungufu ambayo yamekosa utaalamu katika ujenzi wake.
“Sisemi kwa wivu lakini ukweli ni kwamba sebule ya jumba hilo ina eneo kubwa mno lililo wazi ambalo linaondoa uzuri wa jumba hilo,” Sean amesema. “Kutokana na eneo hilo kuwa wazi sehemu kubwa hata kama ukienda kwa sauti ndogo itasikika na mwangwi wa kutisha mno”.
Kibaki ameongeza kuwa ingawa jumba hilo ni la kuvutia, upambaji wa kufikiriwa zaidi unaweza kuifanya iwe ya kuvutia zaidi. “Ni nyumba yako lakini ongeza mimea au kitu cha kuifanya iwe hai hivyo ilivyo haioneshi uhai wa nyumba,” alipendekeza.
Kibaki ameongeza kwamba timu ya Khaligraph inaweza kuwa ilipuuza njia sahihi za wataalamu wa majengo. “Mtu anayewekeza kiasi hicho kwenye jumba kama hilo anapaswa kupata wataalamu wa kuifanya nyumba hiyo iwe na uhai kuanzia kwenye mapambo na namna ya kuiweka kwa ndani. Ila simlaumu kabisa Kaligraph, ni watu walio karibu naye ndio hawakutoa mwongozo ufaao katika ujenzi wa jumba hilo.”
Licha ya wakosoaji hao, Khaligraph ametetea kwa dhati jumba lake, akielezea kama ishara ya safari yake kutoka mazingira duni hadi kupata mafanikio aliyonayo kwa sasa.