Lamata atoa gari mbili kwa Miss Zone na Miss Tanzania

DAR ES SALAAM: MWANDAAJI wa Shindano la Miss Tanzania, Leah Mwendamseke ‘Lamata’, amesema mshindi wa Miss Zone ataondoka na gari, huku mshindi wa taji la Miss Tanzania naye akijinyakulia gari nyingine.
Lamata ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi rasmi wa mashindano ya Miss Tanzania, akibainisha kuwa amedhamiria kuongeza thamani ya shindano hilo na kuwapa warembo fursa ya kutambua vipaji vyao na uwezo wao.
Amesema kila mshindi wa Miss Zone atapatiwa gari, huku mshindi wa shindano la Miss Tanzania akiondoka na gari nyingine, hatua inayotarajiwa kuongeza ushindani na kuwavutia warembo wengi zaidi kujitokeza kuwania mataji hayo.

“Ni wakati wa warembo kujifunza, kujitambua na kuona thamani yao, pamoja na kupata fursa na stahiki kulingana na kile wanachokifanya,” amesema Lamata.
Katika hafla hiyo, Lamata pia aliwatambulisha waandaaji wa mashindano ya Miss Zone pamoja na kueleza zawadi mbalimbali zitakazotolewa kwa washindi.
Kwa upande wake, muigizaji wa filamu, Mama Ashura, amesema mashindano hayo yataendeshwa kwa misingi ya haki na maadili, akisisitiza kuwa hakutakuwa na nafasi ya vitendo vya unyanyasaji, ikiwemo rushwa ya ngono.
Amesema Lamata tayari ameonesha mchango mkubwa katika kupambana na unyanyasaji wa wanawake ndani ya tasnia ya filamu na anaamini msimamo huo utaendelea pia katika mashindano ya urembo.
“Lamata ametukomboa sana kwenye tasnia ya filamu. Sisi wanawake tulikuwa tukinyanyasika, lakini sasa tunafurahia na kuonesha vipaji vyetu kwa uhuru,” amesema Mama Ashura.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwapa warembo fursa ya kuonesha vipaji, kujiamini na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, huku waandaaji wakiahidi kuyasimamia kwa kuzingatia maadili, uwazi na haki kwa washiriki wote.




