Muziki

Marioo apeperushe bendera ya Tanzania AFRIMMA 2026

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Omary Mwanga ‘Marioo’, ameipeperusha vyema bendera ya Tanzania baada ya kutwaa tuzo ya Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki katika tuzo za African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2026, zilizofanyika jijini Dallas, Texas, nchini Marekani.

Marioo aliibuka mshindi katika kipengele hicho baada ya kuwashinda wasanii wengine wakubwa wa Afrika Mashariki, akiwemo Naseeb Abdul maarufu kama Diamond Platnumz, Juma Jux, Mbosso na Barnaba kutoka Tanzania.

Wengine waliokuwa wakishindania tuzo hiyo ni Bien kutoka Kenya, Eddy Kenzo na Joshua Baraka wa Uganda, Lij Michael wa Ethiopia pamoja na Single Dee wa Sudan Kusini.

Ushindi huo ni hatua nyingine kubwa katika safari ya kimuziki ya Marioo na unaendelea kuthibitisha nafasi yake katika muziki wa Bongo Fleva na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Kabla ya tuzo hizo, Marioo alikuwa miongoni mwa wasanii wa Tanzania waliotajwa kutumbuiza katika AFRIMMA Music Fest, iliyofanyika katika ukumbi wa Annette Strauss Square jijini Dallas. Tamasha hilo liliwakutanisha wasanii mbalimbali wa Afrika na mashabiki wa muziki kutoka maeneo tofauti.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kabla ya hafla hiyo, Tanzania ilikuwa na uwakilishi mkubwa katika AFRIMMA 2026, huku wasanii kadhaa wakipata nafasi ya kuwania tuzo katika vipengele mbalimbali.

Tuzo za AFRIMMA hutambua na kuthamini mchango wa wasanii, nyimbo, maonesho pamoja na wadau mbalimbali katika kukuza na kueneza muziki wa Afrika duniani.

Kwa ushindi huo, Marioo ameongeza heshima kwa muziki wa Tanzania na kuendelea kuonyesha kuwa Bongo Fleva ina nafasi kubwa katika jukwaa la kimataifa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button