Tanzania yaweka heshima Kenya

KENYA: WAWAKILISHI wa Tanzania katika mchezo wa kuongelea, timu ya HPT wamefanikiwa kushika nafasi ya tatu ya ushindi wa jumla kati ya klabu zaidi ya thelathini vilivyoshiriki mashindano ya Kenya Aquatics National Swimming Championship 2024 (50m).
Akizungumza na Spotileo, Meneja wa timu hiyo, Francisca Binamungu amesema Kikosi cha wachezaji wanne kimejitahidi na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu ya ushindi wa jumla kati ya vilabu zaidi ya thelathini vilivyoshiriki mashindano hayo ya taifa ya Kenya.
Amesema pamoja na ushindi huo pia wachezaji watatu wameibuka kuwa washindi wa kwanza katika umri tofauti tofauti, Mark Tibazarwa amekuwa mchezaji bora wa wachezaji wa umri wa miaka 14 – 15, huku akijitwalia medali mbili za Shaba, medali tatu za fedha na medali tatu za dhahabu.
“Romeo Mwaipasi ameshinda mchezaji bora kati ya wachezaji wa umri wa miaka 16 – 17, naye amefanikiwa kutwa medali moja ya fedha na medali saba za dhahabu, nafasi ya tatu imechukuliwa na Crissa Dillip amefanikiwa kutwaa medali zote nane za dhahabu na hivyo kuibuka mchezaji bora wa wasichana wenye umri wa miaka 12 – 13.,” amesema Francisca.
Ameeleza mbali na ushindi huo Crissa Dillip amekuwa mshindi wa kwanza katika mbio saba alizoshiriki na kushika nafasi ya pili katika mbio moja tu kwa upande wa wasichana wa umri wote walioshiriki mashindano hayo.
Amesema Delbert Kenemo ambaye, kwa ujumla yeye ndiye aliyefanya vizuri zaidi kwa kufanikiwa kupunguza muda wake katika mbio zake zote alizoshiriki, licha ya ya kuwa na changamoto la kutokuwa na bwana la kuongelea la Mita 50 lakini wachezaji walifanikiwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
“Napenda kutoa shukrani za pekee kwa Serikali kwa kutukabidhi bendera na kutoa maneno ya hamasa kwa wachezaji wetu, ambayo mara zote yamewatia moyo na kuwafanya wapambane zaidi, pili shukrani nyingi ziwaendee viongozi wetu wa chama cha kuogelea (TSA) ambao wamekuwa nasi bega kwa bega toka maandalizi ya safari na mpaka hivi sasa.,” amesema Meneja huyo.
Mashindano hayo ya siku mbili yamefikia tamati huku Tanzania ikiwa ni nchi alikwa katika mashindano hayo ya Taifa ya nchini Kenya.