Chama: Azam ni mechi ngumu

DAR ES SALAAM: KIUNGO wa Simba, Clatous Chama, amesema mchezo dhidi ya Azam FC utakuwa mgumu na kuwataka wachezaji wenzake kuendelea kujiandaa kwa ajili ya pambano hilo litakalochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Chama ametoa kauli hiyo baada ya Simba kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao 6-1 dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa jana, matokeo yaliyoiwezesha timu hiyo kusonga mbele katika hatua inayofuata.
“Azam ni timu nzuri, kila muda tunapokutana na Azam inakuwa mechi ngumu sana. Kwa hiyo naona sasa hivi ni kuendelea kuwa tayari, kufanya mazoezi na kujiandaa kwa mchezo unaokuja,” amesema Chama.
Amesema ushindi huo dhidi ya Mighty Wanderers ulikuwa muhimu kutokana na malengo makubwa waliyokuwa nayo, huku akimshukuru Mungu kwa kuwawezesha kumaliza mchezo salama bila mchezaji yeyote kupata majeraha.
“Tushukuru Mungu tumepata matokeo mazuri na tumeumaliza mchezo salama, hakuna msjeruhi yoyote iliyotokea. Mechi ilikuwa ngumu na ilikuwa na malengo makubwa, kwa hiyo tushukuru Mungu tumekuwa na performance nzuri,” amesema.
Chama pia aliwapongeza wachezaji wenzake kwa mchango wao katika ushindi huo, akisema uwepo wa mashabiki wengi uwanjani uliwapa motisha zaidi ya kupambana hadi kupata matokeo mazuri.




