Nyerere Cycling kupeleka elimu, afya Butiama

Msafara huo wenye urefu wa kilomita 1,500 hadi Butiama, utafanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 14, 2026, ukiwa na mkazo katika elimu, afya na uhifadhi wa mazingira, sambamba na kuhamasisha wanafunzi, hususan wasichana, kushiriki katika michezo ya kuendesha baiskeli.
Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Zuweina Farah, alisema kampuni hiyo itaendelea kuwa mshirika mkuu wa Nyerere Cycling Tour, akieleza kuwa ushirikiano huo unaonesha dhamira ya kampuni kuunga mkono mipango yenye kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Baadhi ya washiriki wa msafara wa Nyerere cycling tour wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari na wadau wa msafara huo uliolenga kutangaza rasmi washirika wa zamani na wapya wa msafara huo.
Alisema Vodacom inafurahia pia kushirikiana na washirika wapya ambao, kwa pamoja, wataongeza thamani katika safari ya mwaka huu na kusaidia kupanua wigo wa matokeo ya msafara huo.
Kwa mujibu wa Vodacom, shughuli za kijamii zitakazotekelezwa mwaka huu zinatarajiwa kuwafikia zaidi ya wanafunzi 25,000, huku katika safari zilizopita msafara huo ukifika katika shule 107 na kunufaisha zaidi ya wanafunzi 75,000.
Meneja wa Uendelevu wa Stanbic Bank Tanzania, Annette Mkini, alisema benki hiyo itatumia msafara huo kuhamasisha elimu ya fedha kwa wanafunzi na vijana, ikiwa ni pamoja na kuwajengea uelewa utakaowasaidia kufanya maamuzi bora kuhusu matumizi na usimamizi wa fedha.

Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour Gabriel Landa (wa kwanza kulia) akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari na washirika wao. Majadiliano hayo yalihusu namna gani watajumuika katika msafara huo.
Kwa upande wake, Afro Oil imesema ushiriki wake unatokana na dhamira ya kampuni ya kurudisha kwa jamii, wakati Samwel Msonsa kutoka BYD alisema kampuni hiyo itashiriki katika uzalishaji na uhamasishaji wa msafara huo, pamoja na shughuli za uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji miti.
Msafara huo hadi sasa umesajili waendesha baiskeli 213, huku wengine wakitarajiwa kujiunga njiani. Waendesha baiskeli kutoka nchi 12 wanatarajiwa kushiriki, huku wanawake 23 tayari wakiwa wamesajiliwa.

Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour Gabriel Landa akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari na wadau wa msafara. Mkutano huo ulilenga kutangaza rasmi washirika wa zamani na wapya wa msafara huo.
Vodacom Tanzania imewekeza Sh milioni 160 katika Msafara wa Baiskeli wa Nyerere, huku Vodacom Foundation ikichangia zaidi ya Sh milioni 300 kwa shughuli za kijamii zitakazotekelezwa katika maeneo yatakayopitiwa na msafara huo.

Washirika, Washiriki na Wadau wa Nyerere Cycling Tour wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kuhitimisha mkutano wa waandishi wa habari uliopangwa kwa ajili ya kutangaza rasmi washirika wapya na wa zamani wa msafara huo.
Safari hiyo itahitimishwa Butiama, mkoani Mara, nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.




