‘Wapigambizi’ wetu kuliwakilisha Taifa Kenya
DAR ES SALAAM: TIMU ya Taifa ya kuogelea mita 50 imeagwa leo jijini Dar Es Salaam kwenda nchini Kenya kushiriki katika mashindano ya kuongelea ya kimataifa ya Kenya Aquatics National Swimming Championships 2024.
Timu hiyo imekabidhiwa bendera jana kwa ajili ya kwenda nchini humo katika kuwakilisha Tanzania katika mashindano hayo ya klabu za kuongelea nchini Kenya.
Akizungumza na Spotileo afisa michezo wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Abel Samweli amesema wanategemea makubwa kutoka kwa timu hiyo inapokwenda nchini Kenya ikiwemo kurejea na medali za kutosha.
“Kikubwa kufanya vizuri tunatarajia washiriki wetu watarejea na medali ya dhahabu licha ya kutambua changamoto ya kuzoea kuongelea bwawa la mita 25 na wanaenda kwenye mita 50,” amesema Afisa huyo.
Naye Mkuu wa msafara na meneja wa timu hiyo, Francisca Dillip, amesema timu imepata mwaliko na wanaondoka kesho kuelekea Kenya katika mashindano yanayofanyika katika uwanja wa Kasarani na kuanza Juni 22 hadi 23 mwaka huu.
“Tunaenda na Wachezaji wanne timu ipo tayari kwa ajili ya mashindano hayo ya Taifa na tunaenda kushindana, licha ya kuwepo kwa changamoto ya wachezaji wetu kuogelea kwenye mita 25 lakini wanaenda kwenye mita 50, tunaamini watafanya vizuri na kurejea na medali “ amesema Francisca.
Naye Kocha wa timu hiyo, Alexander Mwaipasi amesema wamejipanga vizuri kikubwa ni kuomba baraka za watanzania kwenda kufanya vizuri katika mashindano nchini Kenya.
“Mashindano haya ni ya klabu za nchini Kenya lakini Tanzania tumepata mwaliko kwa maandalizi tuliyofanya tunatarajia kurejea na medali ya dhahabu, pia tunaenda kutumia mashindano haya kama daraja kupanda viwango vya kimataifa,” amesema meneja huyo.