Dar Swim Club yajipanga kufanya makubwa Kenya

TIMU ya Kuogelea ya Dar Swim imepania kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa yatakayofanyika nchini Kenya kuanzia Februari 15 hadi 16.
Akizungumza na gazeti hili Kocha wa Dar Swim Kanisi Mabena amesema kwa maandalizi mazuri waliyofanya anaamini watafanya vizuri.
“Mashindano haya ni muhimu kwetu kwenda kuongeza uzoefu, kikosi changu kimejipanga kwa muda mrefu naamini watafanya vizuri,”amesema.
Amesema hana hofu kwasababu wachezaji wengi alionao ni wana uzoefu na mashindano mbalimbali wanachoenda kufanya ni kuendelea kupambana na kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Kikosi cha wachezaji sita kimeondoka Dar es Salaam jana Februari 13, 2025 kuelekea nchini Kenya tayari kupambana na kurudi na medali za ushindi.
Mbali na Dar Swim, timu nyingine za Tanzania zitakazoshiriki ni Reptide ya Arusha na Tanzania Swim Squad yenye wachezaji kutoka klabu tofauti.