Salah afunguka kubaki Liverpool

LIVERPOOL, WINGA wa majogoo wa jiji na nahodha wa timu ya taifa ya Egypt Mohamed Salah amesema uwezekano wa kikosi hicho kutwaa mataji hasa la Ligi Kuu ya England msimu huu ndio sababu kubwa ya kuongeza mkataba wa miaka miwili wa kisalia klabuni hapo mpaka 2027
Salah ambaye amesaini mkataba mpya leo hii na kuzima tetesi za muda mrefu za kuondoka klabuni hapo ameyasema hayo katika mahojiano baada ya kumwaga wino kwenye karatasi za mkataba huku akionekana waziwazi ni mwenye furaha zaidi ya kusalia Liverpool
“Kwakweli ninafuraha sana, tuna timu nzuri sana hivi sasa kama ambavyo tumekuwa na timu bora mara zote. Lakini nimesaini mkataba mpya kwakuwa nadhani tuna nafasi ya kushinda mataji mengine”.
Salah mwenye miaka 32 ameifungia Liverpool magoli 243 katika mechi 394 alizocheza tangu alipowasili England kutoka kutoka Roma mwaka 2017 magoli yanayomfanya kuwa mfungaji bora wa muda wote namba 3 wa klabu hiyo huku akiisaidia Liverpool kumaliza ukame wa miaka 30 bila taji la Ligi Kuu msimu wa 2019/20.
Msimu huu Salah hakamatiki hata kidogo ndiye kinara wa mabao na asisti jumla amehusika na mabao 44 akiisaidia klabu yake kuzidi kulisogelea taji la Premier League msimu huu wakiwa mbele kwa pointi 11 zaidi ya Arsenal aliye katika nafasi ya pili