Haaland aweka rekodi EPL

MSHAMBULIAJI Erling Haaland amekuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 20 mapema zaidi Ligi Kuu England (EPL) katika ushindi wa timu yake Manchester City wa mabao 3-1 dhidi ya Leeds United akifunga mawili.
City ilipata bao la kuongoza dakika chache kabla ya mapumziko kupitia kwa Rodrigo Hernández Cascante ‘Rodri’ wakati wa mchezo huo kwenye uwanja Elland Road.
Akicheza katika mji aliozaliwa wa Leeds dhidi ya timu anayoiunga mkono, Haaland hakushangalia mabao hayo yaliyomuongezea idadi ya aliyofunga katika michezo 14 tu ya ligi aliyocheza.
“Nimekuwa nyumbani, nikiwa na wazimu kwamba sijashiriki Kombe la Dunia. Nimechaji tena betri zangu”, amesema Haaland.
Haaland mwenye umri wa miaka 22 amefunga mabao hayo mawili dakika 51 na 64 akipokea pasi ya Jack Grealish katika mabao yote mawili huku bao pekee la Leeds likifungwa na Pascal Struijk dakika 73.
“Kutazama watu wengine wakifunga ili kushinda michezo kwenye Kombe la Dunia kulinichochea, kulinitia moyo na kuniudhi. Nina njaa zaidi ya kufunga kuliko hapo awali,”ameongeza Haaland.
City sasa ni ya pili katika msimamo wa EPL ikiwa na pointi 35 nyuma ya Arsenal inayoongoza kwa pointi 40 baada ya michezo 15 kila moja zikitengenishwa na tofauti ya pointi tano.