Rodri ndio basi tena!

LONDON, ENGLAND: Sasa ni rasmi kiungo wa Manchester city Rodrigo Cascante ‘Rodri’ atakuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima baada ya kocha mkuu wa kikosi hicho Pep Guardiola kuthibitisha kuwa Rodri atakuwa nje baada ya kupata majeraha ya goti (ACL).
Mhispania huyo alionekana kuchechemea katika kipindi cha kwanza cha sare ya 2-2 kati ya Manchester City na Arsenal baada ya kutokea sintofahamu kati yake na Thomas Partey kwenye kona.
Awali kulikuwa na tetesi zilizodai kuwa Rodri anaweza kuwa nje kwa msimu mzima kutokana na jeraha hilo baya, kabla hajasafiri kuelekea nchini kwao Hispania kwa vipimo na matibabu zaidi.
Akizungumza kabla ya mchezo wao wa kesho Jumamosi dhidi ya Newcastle United kwenye ligi kuu ya England kocha huyo alieleza ukubwa wa jeraha la kiungo huyo.
“Rodri amefanyiwa upasuaji wa goti lake asubuhi ya leo na msimu ujao atakuwa hapa. Msimu huu umekwisha, ni bahati mbaya, tumepata habari hizi mbaya leo lakini mambo haya yanatokea. Tutakuwepo kumuunga mkono katika kupona kwake hatua kwa hatua. ” Guardiola aliwaambia wanahabari.
“Anachotupa hatuna mchezaji kama yeye. Lakini wengine wote kwa pamoja wanaweza kuchukua nafasi ya kile Rodri amefanya tangu kuwasili kwake Manchester. Itatubidi kufanya hivyo kama timu na kutafuta njia ya kucheza mechi nyingi bila mchezaji huyu muhimu sana kwetu.
Rodri mwenye miaka 28 hajapoteza mchezo wowote katika michezo 52 iliyopita ya Ligi Kuu ya England ambayo ameanza. Ameshinda 42 na sare 10 tangu Februari 2023.