VAR, SAOT kuweka mzani sawa kwenye FA

ENGLAND: Shirikisho la soka nchini England FA limesema teknolojia ya usaidizi wa muamuzi kwa njia ya video VAR itaanza rasmi kutumika katika michezo ya raundi ya 5 ya kombe la FA la nchini England.
Taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya shirikisho hilo la soka imeeleza ujio wa matumizi ya teknolojia hiyo ambayo yatakuwa sambamba na ile ya offside yaani Semi-automated offside technology (SAOT)
Maamuzi ya waamuzi hao wa VAR yatatangazwa kwa mashabiki viwanjani katika mechi zote 8 za raundi hiyo ya 5 yakifafanuliwa kwa lugha nyepesi kuwasaidia mashabiki kuyaelewa.
Matumizi ya teknolojia hiyo yanakuja kama mkombozi baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka nchini humo kutokana na kuwepo kwa matukio tata katika raundi iliyopita ya michuano hiyo.
Mechi za raundi ya 5 ya michuano hiyo inatarajia kuanza mwanzoni mwa mwezi machi mwaka huu huku majina makubwa kutoka Ligi Kuu yakivaana na yale ya madaraja ya chini ambapo Manchester City watawakaribisha Plymouth, Nottingham forest watakuwa wenyeji wa Ipswich Town, NewCastle watavaana na Brighton huku Manchester united wakikipiga na Fulham.Cardiff city watakuwa na kibarua kigumu mbele ya Aston Villa huku Crystal Palace wakikipiga na Millwall.