LONDON: Beki wa kulia wa Chelsea ‘the blues’ Reece James ataukosa mchezo dhidi ya Leeicester City hapo kesho baada ya kupata majeraha ya misuli ya paja huku kukiwa na sintofahamu kuhusu lini beki huyo atarejea uwanjani.
Kuumia kwa James ni pigo kwa Chelsea na ni muendelezo wa majeraha yanayomuandama misimu ya hivi karibuni. Ikumbukwe kuwa nahodha huyo wa Chelsea alifanyiwa upasuaji wa misuli ya paja mwezi Desemba mwaka jana hali iliyomkosesha baadhi ya mechi za mwanzo za msimu huu.
Kupitia mitandao yake ya kijamii James amewaachia ujumbe wa matumaini mashabiki wa Chelsea na wapenda soka kwa ujumla, akiwashukuru kwa kumuunga mkono kwenye safari hii ambayo imejaa panda shuka ya kila aina.
“Ujumbe huu ni kwa watu wanaoelewa na kuheshimu kile ninachopitia, nawakushukuru sana kwa sapoti yenu na jumbe za kunitakia nafuu ya haraka. Nataka niwaambie zimeniguza kuliko mnavyoweza kufikiria. Niko sawa, nilishapitia nyakati ngumu, nilishapitia nyakati nzuri hii ni changamoto nyingine ambayo sina budi kuikubali” – amesema Reece James kwenye sehemu ya taarifa yake.
Chelsea watasafiri hadi Leicester jumamosi hii kwenye mtanange utakaopigwa katika dimba la King Power kabla ya kuvaana na Aston Villa nyumbani Stamford bridge Desemba mosi mwaka huu.