Real Madrid yaweka dau nono kwa Gonzalo

MADRID, Hispania: MABINGWA wa Hispania, Real Madrid, wameweka wazi kuwa hawako tayari kumuuza mshambuliaji wao chipukizi Gonzalo Garcia kwa bei yoyote chini ya euro milioni 60 katika dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi.
Gonzalo (22) amekuwa na msimu wa kipekee licha ya kupata muda mchache wa kuanza kikosi cha kwanza, akishindwa kupenya mbele ya nyota wakubwa kama Kylian Mbappe na Vinicius Junior. Katika mechi 34 alizocheza msimu huu, nyingi ameingia akitokea benchi.
Kutokana na ushindani mkubwa ndani ya kikosi hicho, Real Madrid wapo tayari kumruhusu aondoke ili kupata muda zaidi wa kucheza, lakini wamesisitiza kuwa hilo litafanyika tu iwapo klabu itakayomhitaji itatimiza thamani waliyoipanga.
Taarifa zinaeleza kuwa klabu kadhaa barani Ulaya zimeanza kuonesha nia ya kumsajili, zikiwemo kutoka Italia na Ujerumani. Miongoni mwa wanaomuwania ni Borussia Dortmund, ambao wanatajwa kuwa tayari kutoa euro milioni 30 — kiasi ambacho kiko chini ya nusu ya mahitaji ya Madrid.
Hata hivyo, Real Madrid wanaamini kuwa ongezeko la klabu zinazomtaka mchezaji huyo linaweza kusaidia kupata ofa kubwa zaidi, huku wakifikiria pia kuweka kipengele cha kumnunua tena baadaye (buy-back clause) endapo ataondoka.




