Filamu

Denzel Whitaker wa BlackPanther mgeni rasmi Tamasha la ZIFF 2024

ZANZIBAR: STAA wa filamu ya BlackPanther na muandaaji wa filamu mbalimbali kutoka nchini Marekani Denzel Whitaker anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) 2024, litakaloanza Agosti 1 hadi 4 Visiwani Zanzibar.

Tamasha hilo litafanyika katika kumbi mbalimbali za Mji Mkongwe na nje ya mji huo huku wageni maarufu, waigizaji, waongozaji na wazalishaji wa filamu nguli kutoka kote duniani wakitarajiwa kuwepo Zanzibar.

AFISA Mtendaji Mkuu wa Tamasha hilo Joseph Mwale, amesema wapo wageni mbalimbali kutoka nchi mbalimbali watakaoshiriki tamasha hilo lakini Denzel Whitaker ndiye atakayekuwa mgeni rasmi kutokana na mchango wake mkubwa wa kuendeleza filamu, sanaa ya uigizaji na michezo ya jukwaani.

“Tunatarajia kuanza kupokea wageni wengi mashuhuri kutoka kote duniani watakaokuja kwa ajili ya tamasha la ZIFF jambo ambalo ni muhimu mno kwa wasanii wa ndani kama watatumia tamasha hili kama fursa kwao ya kukutana na kujifunza kutoka kwa waigizaji nguli, waongozaji, wazalishaji na wadau wakubwa wa masoko ya filamu ili nao wapenye katika soko la kimataifa, iwe faida kwao na nchi kwa ujumla,” ameeleza Mwale.

Mwale ameongeza kwamba wamepunguza siku za tamasha hilo kutoka 10 hadi 4 ili kuliboresha tamasha hilo; “Tumepunguza siku ili kupunguza gharama zisizo na ulazima lakini pia tumeongeza ufanisi wa tamasha kwa maana uongozi mpya na tamasha limekuwa jipya bila kuondoa misingi yake na atakayehudhuria tamasha hili kwa mwaka huu atakuwa shuhuda na balozi wetu mkubwa kutokana na ubora atakaokutana nao katika tamasha hili”.

Denzel Whitaker amefurahishwa na mwaliko huo na amewataka wapenda filamu, waigizaji, waongozaji, wazalishaji wafike katika tamasha hilo kwa kuwa mambo makubwa yatakwenda kufanyika katika tamasha hilo yatakayoinufaisha tasnina nzima ya filamu kote inakofanyika.

Denzel alianza uigizaji kupitia uchekeshaji kupitia tamthilia ya ‘One on One’ ya mwaka 2001 hadi 2006, ‘The War at Home’ ya mwaka 2005 hadi 2007, filamu ya ‘Training Day’ ya 2001 na nyingine nyingi.

Related Articles

Back to top button