Polisi yatwaa ubingwa, Chaneta yatamba kuibua vipaji

DODOMA:TIMU ya Polisi imeibuka bingwa wa Ligi ya Netiboli Daraja la Kwanza 2026 baada ya kuifunga Uhamiaji Queens mabao 43-36 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Ushindi huo umehitimisha kampeni nzuri ya Polisi iliyodhihirisha ubora, nidhamu na mshikamano katika mashindano hayo yaliyoshirikisha timu mbalimbali kutoka nchini kote.
Wakati ligi hiyo ikifikia tamati, Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kimesema mashindano hayo yameendelea kuwa chachu ya kuibua vipaji vya wachezaji na kuimarisha Timu ya Taifa.
Akisoma risala maalum katika sherehe za kufunga ligi hiyo, Katibu Mkuu wa CHANETA, Rahma Kilimba, amesema Ligi ya Daraja la Kwanza imechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa wachezaji wanaokwenda kuitumikia Timu ya Taifa kutokana na viwango wanavyoonesha katika mashindano hayo.
Kilimba amesema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto zinazokabili maendeleo ya mchezo huo ikiwemo upungufu wa viwanja bora vya mazoezi na mashindano pamoja na ukosefu wa wadhamini wa kudumu watakaosaidia kuendeleza netiboli nchini.
Risala hiyo iliwasilishwa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabiri Shekimweri, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma katika hafla ya kufunga mashindano hayo.
CHANETA imeeleza matumaini kuwa kupitia maboresho ya miundombinu na kuongezeka kwa uwekezaji katika mchezo huo, netiboli itaendelea kuibua vipaji vingi zaidi na kuongeza ushindani katika ngazi ya taifa na kimataifa.




